Mazungumzo ya amani ya Tigray kufanyika Oktoba 24 Afrika Kusini
(last modified Fri, 21 Oct 2022 04:12:40 GMT )
Oct 21, 2022 04:12 UTC
  • Mazungumzo ya amani ya Tigray kufanyika Oktoba 24 Afrika Kusini

Mazungumzo ya amani ya kujaribu kutatua mgogoro katika eneo la Tigray huko kaskazini mwa Ethiopia kati ya serikali kuu na wapiganaji wa TPLF yameratibiwa kufanyika wiki ijayo.

Redwan Hussein, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed amesema, "Kamisheni ya Umoja wa Afrika imetujulisha kuwa, Mazungumzo ya Amani yatafanyika Oktoba 24 nchini Afrika Kusini."

Mazungumzo hayo ya amani baina ya waasi wa TPLF na serikali ya Ethiopia kwa usimamizi wa mjumbe wa Umoja wa Afrika, Olusegun Obasanjo, aliyekuwa Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Phumzile Mlambo-Ngcuka na aliyekuwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta yalitazamiwa kufanyika siku chache zilizopita, lakini yakaakhirishwa kwa sababu za kilojistiki.

Haya yanajiri baada ya Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutoa wito wa kusitishwa mapigano katika jimbo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia ambako amesema kuwa hali ya mambo inaendelea kuzorota na kushindwa kudhibitika.

Mgogoro wa kibinadamu katika eneo la Tigray

Alisema vita vinapaswa kuhitimishwa sasa huko Tigray ikiwa ni pamoja na kuondoka haraka iwezekanavyo wanajeshi wa Eritrea katika eneo hilo. Kabla ya hapo pia, Umoja wa Afrika (AU) ulitoa wito wa kusitishwa mapigano haraka iwezekanavyo huko Tigray. 

Machafuko na vita vilivyoshuhudiwa katika eneo la Tigray huko kaskazini mwa Ethiopia kati ya jeshi la serikali kuu na wapiganaji wa kundi la waasi la TPLF tokea Novemba 2020 vimepelekea kuuliwa makumi ya maelfu ya watu na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.