Mafuriko yasababisha watu milioni 3.4 kupoteza makazi yao magharibi, katikati mwa Afrika
(last modified Sat, 29 Oct 2022 04:20:11 GMT )
Oct 29, 2022 04:20 UTC
  • Mafuriko yasababisha watu milioni 3.4 kupoteza makazi yao magharibi, katikati mwa Afrika

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limesema mamilioni ya watu wamepoteza makazi yao katika nchi za magharibi na katikati mwa Afrika kutokana na mafuriko.

Taarifa ya jana Ijumaa ya UNHCR imesema kuwa, mafuriko ya sasa ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, yameua mamia ya watu na kuwaacha wengine milioni 1.3 bila makazi nchini Nigeria, mbali na kuathiri watu milioni 2.8 katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi. 

Kwa mujibu wa Msemaji wa Idara ya Kushughulikia Majanga nchini Nigeria, Manzo Ezekiel, mbali na watu zaidi ya 500 kufa maji, wengine zaidi ya milioni 1.4 wameachwa bila makazi baada ya nyumba zao kusombwa na maji ya mafuriko hayo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi limesema katika taarifa ya Ijumaa kuwa, mafuriko hayo yameathiri pia watu milioni moja nchini Chad.

Kwa mujibu wa taasisi hiyo ya UN, mafuriko hayo mbali na kuua mamia ya watu, lakini pia yamewaacha maelfu ya watu bila makazi katika nchi za Niger, Mali na Burkina Faso.

Sudan pia imekumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha karibuni

Olga Sarrado, Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi amesema kuna uhusiano wa wazi kati ya mabadiliko ya tabianchi na watu kuachwa bila makazi katika majanga hayo ya kimaumbile yanayoshuhudiwa katika maeneo ya magharibi na katikati ya Afrika.

Huku eneo la Afrika Magharibi likishuhudia mvua kubwa za mafuriko, kinaya ni kuwa eneo la Pembe ya Afrika linashuhudia ukame na kiangazi ambacho hakijawahi kushuhudiwa ndani ya miaka 40 iliyopita.