Nov 02, 2022 02:47 UTC
  • Mahakama ya Jamhuri ya Afrika ya Kati yawahukumu kifungo wanamgambo 3 kwa jinai dhidi ya binadamu

Mahakama Maalumu inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati imewapata na hatia wanamgambo watatu kwa kutenda jinai dhidi ya binadamu na kuwahukumu vifungo vya jela kuanzia miaka 20 hadi vifungo vya maisha.

Issa Sallet Adoum, Ousman Yaouberms Rangia na Tahir Mahamat walikuwa wakituhumiwa kushiriki katika mashambulizi ya kundi la wanamgambo wanaobeba silaha la "3R" mnamo mwezi Mei mwaka 2019; ambapo wanavijiji 46 waliuliwa kwa umati huko kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Katika kesi ya kwanza kuwahi kusikilizwa na Mahakama Maalumu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, kikao cha mahakama kilichowajumuisha majaji wa ndani ya nchi hiyo na wa kimataifa kimemhukumu Issa Sallet Adoum kifungo cha maisha jela na kuwakatia wengine hukumu ya kifungo cha miaka 20. 

Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo inahesabiwa kuwa moja kati ya nchi maskini sana na iliyoathiriwa pakubwa na machafuko duniani, ilitumbukia katika vita vya ndani mwaka 2013. Kundi la "3R ni mojawapo ya makundi ya wanamgambo yenye nguvu kubwa na wanachama wake wengi wanatoka katika kabila la Fulani. 

Wanamgambo wa kundi la "3R " wa Jamhuri ya Afrika ya Kati 

Jukumu kuu la Mahakama Maalumu inayoungwa mkono na UUN ni kusikiliza na kutoa hukumu za kesi za uhalifu wa kivita na jinai dhidi ya binadamu zilizotekelezwa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati tangu mwaka 2003. Mahakama hiyo iliundwa mwaka 2015 kwa uungaji mkono wa Umoja wa Mataifa; hata hivyo ilikabiliwa na vizuizi mbalimbali kwa miaka kadhaa kama vile vya kilojistiki, ukosefu wa fedha na upinzani wa ndani. 

Tags