Watu 15 wauawa katika shambulio la kigaidi nchini Somalia
Kwa akali watu 15 wameuawa katika shambulio jingine la kigaidi lililolenga kambi ya mafunzo ya kijeshi karibu na Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.
Raia na makurutu wapya wa kijeshi ni miongoni mwa watu waliouawa katika hujuma hiyo ya jana jioni, baada ya gaidi aliyejifunga mabomu kujiripua katika kambi hiyo iliyoko katika wilaya ya Wadjar, kusini mwa Mogadishu.
Shirika rasmi la habari la Somalia limetoa taarifa ya kulaani shambulio hilo lililolitaja kuwa la kioga dhidi ya watu wasio na hatia, ambalo kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limetangaza kuhusika nalo.
Genge hilo la kigaidi limekiri kupoteza wanachama wake wanane kwenye shambulio hilo, huku likidai kuwa limefanikiwa kuua watu 36 kambini hapo.
Haya yanajiri siku moja baada ya Wizara ya Ulinzi ya Somalia kusema kwamba wanajeshi wa serikali wakiungwa mkono na vikosi vya wanamgambo wa koo vinavyojulikana kama macawisley au "wanaume wenye vikoi," waliwaua magaidi zaidi ya 100 wa al-Shabaab katika mapigano makali katika eneo la kati la Hiran.
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi Abdullahi Ali Anod amesema mapigano makali kati ya pande hizo mbili yalitokea siku ya Alhamisi katika vijiji vya Garas Magan na El Hareeri.
Aidha shambulio hilo la jana jioni linajiri siku chache baada ya kutokea milipuko miwili ya mabomu iliyosababisha vifo vya takriban watu 120 katika mji mkuu, Mogadishu. Magaidi wa al-Shabaab walidai kuhusika na miripuko hiyo nje ya Wizara ya Elimu huko Mogadishu mnamo Oktoba 29.