Wanamgambo wa al-Shabab washambulia kambi ya jeshi nchini Somalia
Kundi la kigaidi la wanamgambo wa al-Shabab limeshambulia kambi moja ya jeshi katikati ya mji wa Galgaduud nchini Somalia.
Wizara ya Ulinzi ya Somalia imetangaza kuwa, shambulio hilo limefanywa leo na wanamgambo hao ikiwa ni siku chache tu baada ya kutwaliwa na vikosi vya serikali.
Hadi sasa haijafahamika hasara au idadi ya watu waliojeruhiwa auu kuuawa katika shambulio hilo la kigaidi la wanamgambo wa al-Shabab.
Shambulio hilo limekuja siku moja tu baada ya kwa akali watu 15 kuuawa katika shambulio jingine la kigaidi lililolenga kambi ya mafunzo ya kijeshi karibu na Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya Wizara ya Ulinzi ya Somalia kusema kwamba wanajeshi wa serikali wakiungwa mkono na vikosi vya wanamgambo wa koo vinavyojulikana kama macawisley au "wanaume wenye vikoi," waliwaua magaidi zaidi ya 100 wa al-Shabaab katika mapigano makali katika eneo la kati la Hiran.
Magaidi wakufurishaji wa al-Shabab wameua makumi ya maelfu ya watu tangu 2006 wakati walipoanzisha kampeni yao chafu kwa kueneza ugaidi miongoni mwa raia ili kupindua serikali kuu ya Somalia inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Kikosi cha Umoja wa Afrika kimefanikiwa kuwatimuwa magaidi wa al-Shabab nje ya mji mkuu, Mogadishu mwaka 2011, lakini kundi hilo bado linadhibiti maeneo mengi ya mashambani na mara kwa mara hufanya mashambulizi ya bunduki na mabomu dhidi ya raia na wanajeshi.
Somalia ni nchi maskini ambayo sasa pia inakabiliwa na ukame mbaya ambao umepelekea watu milioni moja kukimbia makwao.