Wanamgambo waua wanakijiji 12 kaskazini mwa Nigeria
Watu wenye silaha nchini Nigeria wameshambulia kijiji kimoja na kuwaua watu wasiopungua 12 katika shambulizi jipya huko kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.
Gavana wa jimbo la Plateua la kaskazini mwa Nigeria, Simon Bako Lalong amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa, mbali na wanakijiji 12 kuuawa, wengine kadhaa wamejeruhiwa katika shambulio hilo jipya.
Wakazi wa eneo hilo wamesema hujuma hiyo ya jana ni muendelezo wa wimbi la mashambulizi ya hivi karibuni ya magenge yenye silaha ambayo yamekuwa yakivamia vijiji, ni yale yaliyotokea katika shule na barabara kuu.
Haya yanajiri siku chache baada ya genge jingine la wanamgambo kuwateka nyara takriban watu 80 na kuwaua wengine 11 katika mashambulizi tofauti huko kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.

Aidha mapema mwezi huu, wabeba silaha waliwateka nyara takriban watoto 39, wengi wao wakiwa wasichana, waliokuwa wamekwenda shambani kuvuna mazao kwa ajili ya malipo huko kaskazini magharibi mwa Nigeria.
Ukosefu wa usalama umeongezeka nchini Nigeria hivi sasa wakati nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ikikaribia kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwezi Februari 2023.