AU: Kundi la al-Shabaab linaelekea kusambaratika nchini Somalia
Umoja wa Afrika umesema vitendo vya hivi karibuni vya kundi la kigaidi la al-Shabaab vya kuwalenga raia wasio na hatia katika mashambulizi yao vinaashiria namna genge hilo lilivyopoteza udhibiti wa ngome zake, kutokana na operesheni za Jeshi la Taifa la Somalia (SNA) na waitifaki wake.
Sanjari na kulaani shambulio la hivi karibuni la al-Shabaab dhidi ya hoteli moja mashuhuri mjini Mogadishu, Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) kimesema wanamgambo hao wapo katika ncha ya kutokomezwa, na ndiposa wamegeukia mbinu za kipumbavu na kioga za kuwashambulia raia.
Shambulio na mzingiro huo wa siku moja wa wapiganaji wa al-Shabaab uliua watu tisa kwenye jengo lililoko karibu na makazi ya rais katika hoteli ya Villa Rays,katika mji mkuu Mogadishu.
Mwenyekiti wa Baraza la Umoja wa Afrika na kiongozi wa kikosi cha ATMIS, Balozi Mohamed al-Amin Seyf amesema mashambulizi hayo ya kuogofya dhidi ya raia kwa mara nyingine yanaonesha haja ya kuchukuliwa hatua madhubuti dhidi ya ugaidi.
Amesema AU inatoa mkono wa pole kwa familia zilizopoteza watu wao kwenye shambulio hilo la Jumapili, huku ikiwatakia afueni ya haraka majeruhi wa hujuma hiyo ya kigaidi iliyofanywa na wanachama wa al-Shabaab.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Somalia, Hamza Abdi Barre, magaidi zaidi ya 500 wa al-Shabaab wameangamizwa katika operesheni za hivi karibuni na vikosi vya Somalia na waitifaki wake ndani ya miezi minne iliyopita.