UN: Waliouawa Tigray, Ethiopia ni wengi zaidi ya waliouawa Ukraine
(last modified Fri, 09 Dec 2022 02:38:08 GMT )
Dec 09, 2022 02:38 UTC
  • UN: Waliouawa Tigray, Ethiopia ni wengi zaidi ya waliouawa Ukraine

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema idadi ya watu waliouawa katika mapigano huko Tigray, kaskazini mwa Ethiopia ni wengi ikilinganishwa na idadi ya waliouawa katika vita vya Ukraine na Russia.

Antonio Guterres amesema hayo katika hotuba yake kwa Mkutano wa 15 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Kimataifa kuhusu Bioanuai- COP15 unaofanyika Montreal nchini Canada.

Amebainisha kuwa, ingawaje hakuna takwimu rasmi na sahihi juu ya idadi ya watu waliouawa katika mapigano ya miaka miwili huko Tigray, lakini vita hivyo vimepelekea kutengana kwa familia, kuuawa maelfu ya watu na kuachwa mamilioni ya wengine bila makazi.

Guterres ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuunga mkono makubaliano ya amani yaliyofikiwa Novemba 2 kati ya serikali ya Ethiopia na wapiganaji wa Harakati ya Kupigania Ukombozi wa Eneo la Tigray TPLF.

Katibu Mkuu wa UN amefafanua kwa kusema: Makubaliano hayo ya amani ni fursa ambayo Ethiopia, Afrika na dunia kwa ujumla haipaswi kuipoteza. 

Mgogoro wa kibinadamu eneo la Tigray

Umoja wa Afrika umezionya pande husika kwenye makubaliano hayo ya amani kuwa, yoyote atakayekiuka mapatano hayo, atakabiliwa na matokeo mabaya.  

Eneo la Tigray lililoko kaskazini mwa Ethiopia limekuwa likishuhudia mzozo na mapigano kati ya wanamgambo wa kundi la TPLF na jeshi la nchi hiyo tangu Novemba 2020. Maelfu ya raia wameuawa na wengine takribani milioni mbili wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano hayo.