Wakimbizi wa DRC nchini Rwanda wakosoa kimya cha jamii ya kimataifa
(last modified Tue, 13 Dec 2022 07:16:16 GMT )
Dec 13, 2022 07:16 UTC
  • Wakimbizi wa DRC nchini Rwanda wakosoa kimya cha jamii ya kimataifa

Maelfu ya wakimbizi raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walioko nchini Rwanda wameikosoa jamii ya kimataifa kwa kufumbia macho mauaji yanayoendelea kufanywa na magenge ya waasi mashariki mwa DRC.

Maelfu ya wakimbizi hao jana Jumatatu walikusanyika mjini Kigali katika maandamano ya kulalamikia kimya cha jamii ya kimataifa mkabala wa umwagaji damu unaofanywa na magenge ya waasi wakiwemo wa M23 mashariki mwa Kongo DR.

Wakimbizi hao Wakongomani wanaoshi katika Kambi ya Wakimbizi ya Kigeme walikuwa wamebeba mabango yenye jumbe za kuzikosoa taasisi za kimataifa kwa kupuuza mauaji ya halaiki dhidi ya jamaa zao wanaozungumza Kinyarwanda nchini DRC.

Mmoja wa waandamanaji hao amesikika akifoka kwa hasira akisema: Tunalaani kimya na unafiki wa jamii ya kimataifa juu ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi nchini DRC.

Faustin Kalisa, mkimbizi Mkongomani anayeishi nchini Rwanda na aliyeshiriki pia katika maandamano ya jana amenukuliwa akisema, "Tunalaani mauaji ya kimbari yanayoendelea. Tunaishi maisha magumu ya ukimbizi, na jamaa zetu nyumbani (DRC) wanauawa. Ni hali ya kutiwa wasiwasi, na hatujui itaendelea hadi lini."

Wapiganaji wa M23

Wakongomani wanaozungumza Kinyarwanda wanaunda asilimia 5 ya wakazi wote wa mikoa ya Kivu Kusini na Kivu Kaskazini nchini Kongo DR.

Haya yanajiri siku chache baada ya mamlaka za DRC kutangaza kuwa, raia zaidi ya 300 wameuawa katika mashambulizi ya hivi karibuni ya waasi wa M23 katika mji wa Kishishe, mkoani Kivu Kaskazini.

 

Tags