Maiti 27 za wahajiri zapatikana jangwani nchini Chad
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limetangaza habari ya kugunduliwa maiti za wahamiaji 27 zikiwemo za watoto wanne katika jangwa moja nchini Chad.
Anne Kathrin Schaefer, Mkuu wa IOM nchini Chad amesema, wahajiri hao waliondoka katika mji wa Moussoro, magharibi mwa Chad yapata mwaka mmoja na nusu iliyopita wakiwa wamebebwa kwenye gari aina ya pick-up.
Schaefer amesema inaaminika kuwa, wahajiri hao walikwama ndani kabisa ya jangwa baada ya gari lao kuharibika, na yumkini waliaga dunia kutokana na makali ya njaa na kiu.
Taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema, wahajiri zaidi ya 5,600 wameaga dunia wakijaribu kulivuka Jangwa la Sahara katika kipindi cha miaka minane iliyopita, wakiwemo zaidi ya 150 mwaka huu.
Chad imerekodi vifo 110 vya wahamiaji waliojaribu kulivuka jangwa hilo katika kipindi hicho, wakiwemo 27 walioaga dunia hivi karibuni.
Haya yanajiri siku chache baada ya Idara ya Polisi Zambia kugundua miili ya watu 27, wanaoaminika kuwa wahamiaji kutoka Ethiopia, ikiwa imetupwa kwenye eneo moja la shambani kwenye viunga vya mji mkuu, Lusaka.
Kwa mujibu wa IOM, idadi ya vifo vya watu wanaotafuta hifadhi imeongezeka kwa kiasi kikubwa kwenye njia za nchi kavu na baharini kuelekea Ulaya ikilinganishwa na mwaka jana.
Takwimu za Shirika la Kimataifa la Uhamiaji zilizotolewa mwishoni mwa mwezi uliopita zinaonesha kuwa, watu wasiopungua 5,684 wamefariki dunia wakijaribu kukimbilia Ulaya kati ya Agosti 2021 na Septemba mwaka huu.