Wananchi wa Tunisia wapiga kura katika uchaguzi wa bunge uliosusiwa na wapinzani
Wananchi wa Tunisia jana Jumamosi walianza kupiga kura katika uchaguzi wa kwanza wa wabunge tangu Rais Kais Saied atangaze hatua za kipekee Julai 25 mwaka jana baada ya kulifuta kazi Bunge na kutwaa madaraka yote ya nchi. Vyama vya kisiasa na makundi ya upinzani yamesusia uchaguzi huo.
Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa mapema asubuhi ambapo raia wa nchi hiyo wasiopungua milioni 9.3 waliotimiza masharti walitazamiwa kushiriki katika uchaguzi huo kuwachagua wabunge 161 kati ya wagombea 1058.
Mfumo wa uchaguzi wa Tunisia umefanyiwa marekebisho makubwa tangu Rais Kais Saied alipowasilisha katiba mpya kwenye kura ya maoni iliyofanyika mapema mwaka huu. Kwa mujibu wa sheria hizo mpya, vyama vya siasa vya Tunisia haviwezi kufanya kampeni au kufadhili wagombea wao na wagombea wote wanapasa kugombea kama watu binafsi.
Vyama 12 vya siasa kikiweko chama cha Kiislamu cha Ennahda na kile cha mrengo wa kulia cha Qalb Tounes ambavyo kwa pamoja vilikuwa vikiunda muungano mkubwa katika bunge lililovunjwa, vimetangaza kususia uchaguzi huo wa bunge. Wakati huo huo Jumuiya ya Wafanyakazi yenye nguvu ya Tunisia (UGTT) pia imesema inapinga muundo huo wa uchaguzi kwa ujumla.
Kais Saied mhadhiri wa zamani wa taaluma ya sheria ambaye alikuwa mwasiasa wa kujitegemea alipochaguliwa kuwa Rais wa Tunisia, mwaka 2019 alilivunja bunge na kuanza kuongoza Tunisia baada ya kutoa dikrii mwezi Julai mwaka jana; na hatua kwa hatua akaanza kuhodhi madaraka ya nchi hiyo.