Iran ni mwenyeji wa wanafunzi zaidi ya laki saba wa kigeni
Kuna wanafunzi zaidi ya laki saba (700,000) wa kigeni katika shule, taasisi za kielimu na Vyuo Vikuu vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Hayo yalisemwa jana Alkhamisi na Majid Abdollahi, Naibu Mkuu wa Shirika la Ustawi, Ukarabati na Kuzipa Suhula Shule za Iran (DRES) na kuongeza kuwa, katika jumla ya wanafunzi milioni 16.182 waliopo hapa nchini Iran, 700,000 miongoni mwao ni wa kigeni.
Afisa huyo wa Wizara ya Elimu ya Iran ameeleza kuwa, aghalabu ya wanafunzi wa kigeni hapa nchini Iran ni raia wa Afghanistan, ambao wameenea katika mikoa ya Razavi Khorasan, Qom, Semnan, Fars na Sistan na Baluchestan huko kaskazini mashariki, katikati, kusini na kusini mashariki mwa Iran.
Amesema Shirika la Ustawi, Ukarabati na Kuzipa Suhula Shule za Iran (DRES) litaendelea kutumia rasimali zake kujenga shule maalumu kwa ajili ya wanafunzi wa kigeni, kwa kuzingatia miongozi ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR).
Hivi karibuni, Mohammad-Javad Salmanpur, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Anayehusika na Masuala ya Sayansi alisema Iran ni miongoni mwa nchi 15 duniani zenye kuvutia idadi kubwa ya wanafunzi wa kigeni.
Alisema Vyuo Vikuu vya Iran vinapokea idadi kubwa ya wanafunzi kutoka nchi mbalimbali duniani, ikilinganishwa na vyuo vingine hasimu katika eneo la Asia Magharibi na hata barani Ulaya.