Eritrea yadai kuwa imeua askari 200 wa Ethiopia
Eritrea imedai kuwa imeua mamia ya askari wa Ethiopia katika mapigano mapya yanayoendelea katika mpaka wa nchi mbili hizo za Pembe ya Afrika.
Shirika la habari la AFP limenukuu taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Eritrea iliyosema kuwa, jeshi la nchi hiyo limeua askari 200 wa Ethiopia katika mapigano hayo na kujeruhi wengine 300. Hata hivyo taarifa hiyo ya serikali ya Asmara haijabainisha iwapo kuna askari wa nchi hiyo waliouawa au kujeruhiwa katika mapigano hayo. Hadi tunaenda mitamboni serikali ya Ethiopia ilikuwa haijatoa kauli ya kukiri au kukanusha habari za kuuawa mamia ya askari wake.
Hii ni katika hali ambayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema anatiwa wasiwasi na mapigano ya mpakani kati ya Ethiopia na Eritrea. Ban Ki-moon amezitaka Addis Ababa na Asmara kujiepusha na hatua zozote zinazoshadidisha hali ya mivutano kati ya nchi mbili hizo na kusisitiza kuwa, nchi mbili hizo jirani zinapasa kutatua hitilafu zao kwa njia ya amani na kutekeleza makuballiano ya amani yaliyosainiwa na nchi mbili hizo mwaka 2000.
Serikali ya Ethiopia imeyataja mapigano hayo kuwa makali zaidi kuwahi kujiri katika miaka ya hivi karibuni kati yake na Eritrea. Kabla ya mapigano hayo yalioanza Jumapili iliyopita, Ethiopia na Eritrea zimewahi kuingia vitani tena kutokana na mzozo wa mpaka kuanzia mwaka 1998 hadi 2000, ambapo watu zaidi 80,000 waliuawa.