Feb 09, 2023 12:05 UTC
  • Mapigano yashtadi Somaliland, waliouawa wapindukia 70

Idadi ya watu waliouawa katika mapigano yanayoendelea kushuhudiwa kwa siku ya nne hii leo katika mji wa Las Anod, mashariki mwa eneo la Somaliland nchini Somalia imeongezeka na kufikia watu 70.

Duru za hospitali katika mji wa Las Anod zimeliambia shirika la habari la Anadolu kuwa, idadi ya wahanga wa mapigano baina ya maafisa usalama na makundi ya kikabila yaliyoanza tangu Jumatatu iliyopita imefikia watu 70 wakiwemo watoto wadogo.

Fartun Ismail Ahmed, mkazi wa mji wa Las Anod amenukuliwa na Anadolu akisema kuwa, uvurumishaji wa maroketi na maguruneti umeshuhudiwa katika mji huo, huku makazi ya watu, hospitali na maeneo ya ibada yakilengwa na kuharibiwa.

Mapigano hayo yalianzia mjini Lasanod, makao makuu ya eneo la Sool katika jimbo hilo baada ya wanasiasa, makundi ya kiraia na viongozi wa kidini kutagaza kuwa hawataimbua serikali ya Somaliland.

Katika taarifa, viongozi hao wa kisiasa, kidini na kiraia walisema kuanzia sasa jimbo la Somaliland litaongozwa na serikali kuu ya Mogadishu na kwamba serikali ya Somaliland haina uhalali wa kisheria.

Wakazi wa mji wa Las Anod Somaliland wakiswalia maiti

Mapema mwezi uliopita, watu wasiopungua 20 aghalabu yao wakiwa ni raia waliuawa katika mapigano mengine baina ya waandamanaji na maafisa usalama katika eneo la Somaliland. 

Somaliland ilijitenga na Somalia mwaka 1991 lakini haitambuliwi kimataifa. Eneo hilo limekuwa na amani zaidi huku maeneo mengine ya Somalia yakiwa kwenye miongo mitatu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Tags