Wakuu wa Anglikana Afrika watishia kujitenga na UK kwa kubariki ushoga
Viongozi wa Kanisa la Kianglikana barani Afrika wametishia kujitenga na Kanisa la Uingereza kwa kubariki na kuruhusu ndoa na mahusiano ya watu wenye jinsia moja.
Uamuzi huo wa Kanisa la Uingereza wa Februari 9 wa kuwaruhusu viongozi wa Kiangilikana kubariki ndoa za kiraia za watu wenye jinsia moja umekosolewa vikali na wakuu wa kanisa hilo katika nchi za Afrika zikiwemo Kenya, Nigeria, na Uganda.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini Uganda, Stephen Samuel Kaziimba Mugalu amesema: Sisi kama Kanisa la Uganda hatuwezi kuunga mkono uamuzi huo, Mungu hawezi kubariki kitu ambacho amekitaja kuwa ni dhambi.
Awali, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini Kenya, Jackson Ole Sapit alitoa taarifa ya kulaani vikali hatua hiyo ya Kanisa la Uingereza ya kubariki ndoa za watu wenye jinsia moja akisisitiza kuwa, kitendo hicho kimetokana na kuibuka kwa wimbi la uliberali uliokengeuka miongoni mwa wakuu na wafuasi wa kanisa hilo.
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini Nigeria, Henry Chukwudum Ndukuba amesema, "Historia inakaribia kujakariri. Lazima tuufagie uongozi ovu unaobariki dhambi na kuwapotosha wafuasi wa Kanisa la Anglikana kote duniani."
Haya yanajiri huku viongozi mbalimbali wa kisiasa na kijamii pia barani Afrika wakipinga na kukosoa mashinikizo hayo ya Wamagharibi ya kutaka dunia ikumbatie ufuska huo wa mahusiano wa watu wenye jinsia moja.
Miongoni mwao ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye amesisitiza kwa mara nyingine tena kwamba, nchi yake haitaunga mkono vitendo vichafu vya mapenzi ya watu wa jinsia moja, na kwamba, nchi za Magharibi zinapaswa kuacha kutwishana misimamo na mitazamo yao; na kulazimisha nchi zinazopinga kukumbatia vitendo hivyo ambavyo ni kinyume na maadili, vinakinzana na utamaduni wa Kiafrika na ni kinyume na maumbile ya mwanadamu.