Wanadiplomasia wa kigeni wanaoingilia masuala ya ndani Tunisia waonywa
Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia imewaonya vikali wanadiplomasia wa nchi za kigeni wanaoingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Taarifa iliyotolewa jana Jumanne na wizara hiyo imeeleza kuwa, wanadiplomasia wa nchi ajinabi walioko nchini humo wanapasa kuheshimu Hati ya Vienna Kuhusu Mahusiano ya Kigeni, inayowataka waheshimu sheria za nchi walikotumwa, na kutoingilia masuala ya ndani ya nchi husika.
Indhari hii imetolewa kufuatia wimbi la kukamatwa shakhsia na viongozi watajika wa kisiasa na kijamii, ambapo baadhi yao walikuwa na mawasiliano na wanadiplomasia wa nchi za kigeni zinazodaiwa kuingilia masuala ya ndani ya Tunisia.
Hivi karibuni, polisi nchini Tunisia iliwatia mbaroni viongozi kadhaa watajika wa upinzani nchini humo akiwemo Jaouhar Ben Mbarek, mmoja wa wakosoaji wakuu wa Rais Kais Saied.
Aidha Issam Chebbi, kiongozi wa chama cha al-Jamhouri naye alitiwa mbaroni majuzi na anaendelea kushikiliwa na vyombo vya usalama. Hali kadhalika viongozi kadhaa wa chama kikuu cha upinzani cha Ennahdha wamekamatwa pia wakiandamwa na tuhuma mbalimbali.
Kamata kamata hiyo ya vyombo vya usalama dhidi ya wapinzani inaripotiwa katika hali ambayo, mwezi uliomalizika wa Februari, serikali ya Tunisia iliamuru kufukuzwa kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Barani Ulaya, Esther Lynch, kufuatia kushiriki kwake katika maandamano dhidi ya serikali yaliyaoandaliwa na chama kikuu cha wafanyakazi cha Tunisia.