Rais Samia wa Tanzania: Wapinzani si maadui wa taifa
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameendelea kuukumbatia upinzani na kusisitiza kuwa, wapinzani si maadui wa taifa, bali ni nguzo muhimu ya demokrasia ya nchi hiyo. Serikali ya mtangulizi wake hayati John Magufuli ilikuwa inatuhumiwa kuwawekea mbinyo wakosoaji na viongozi wa upinzani.
Rais Samia Suluhu Hassan amesema hayo leo na kueleza kuwa, kabla ya kurejea nchini kwa Mwenyekiti wa chama cha upinzani Chadema, Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, alimtaarifu nia yake hiyo na kumruhusu kurejea pamoja na kufuta kesi zake.
“Mdogo wangu Lema amerudi, aliniambia anataka kurudi nikamwambia rudi, akasema mama nina kesi, nikasema nazifuta rudi.” amesema Rais Samia akiwa Arusha kwenye ziara yake.
Rais Samia amesema hawachukulii viongozi wa vyama upinzania kama maadu na kufafanua kuwa, “Nawachukulia kama watu watakaonionesha changamoto zilizopo nizitekeleze, ili CCM iimarike."
Rais Samia ameongeza kwa kusema, “Mwanaume ni yule anayejiamini, mwanamke ni yule anayejiamini, kwa hiyo kwenye uwanja wa siasa tunajiamini, tuko vizuri na tutakwenda vizuri.”

Mapema mwaka huu, Mama Samia alikutana na viongozi wa vyama 19 venye usajili kamili wa siasa nchini humo Ikulu jijini Dar es Salaam na kusisitiza kuwa, ni haki kwa vyama vya siasa kuendesha mikutano yao ya hadhara nchini humo lakini kuna wajibu wa kila mmoja na upande wa Serikali kuhakikisha mikutano hiyo inafanyika salama.
Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa (OHCHR) ilipongeza hatua hiyo ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutangaza kuondoa marufuku kwa vyama vya siasa nchini humo kufanya mikutano ya hadhara.
Mwishoni mwa Januari mwaka huu, kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu alirejea nyumbani pia kutoka uhamishoni baada ya Mama Samia kuondoa marufuku ya mikutano ya kisiasa ya hadhara.