Upinzani Tunisia wataka kuachiwa huru wafungwa wa kisiasa
Mrengo mkubwa zaidi wa upinzani huko Tunisia umetaka kuachiwa huru wafungwa wa kisiasa huku mgogoro wa kisiasa ukizidi kupanuka katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Wafuasi wa Jumuiya ya Uokovu wa Kitaifa (NSF) jana Jumatano walifanya maandamano katika mji mkuu Tunis, wakiitaka serikali ya Rais Kais Saied iwaachie huru mara moja na bila masharti wakosoaji wa sera zake waliotiwa nguvuni.
Waandamanaji hao walikuwa wamebeba picha za wanachama wa mrengo huo wa upinzani, akiwemo mwanachama Chaima Issa, Waziri Mkuu wa zamani, Ali Laarayedh na Issam Chebbi, Katibu Mkuu wa Chama cha Rebuplican.
Abdellatif Mekki, Katibu Mkuu wa Chama cha Leba na Mafanikio ameuambia umati wa waandamanaji kuwa, "Tunasimama pamoja na wafungwa wa kisiasa."
Aidha mapema jana maandamano mengine yalifanywa na kundi la Wanawake Dhidi ya Ukatili likishinikiza pia kuachiwa huru wafungwa wa kisiasa nchini humo.
Hivi karibuni, polisi nchini Tunisia iliwatia mbaroni viongozi kadhaa watajika wa upinzani nchini humo akiwemo Jaouhar Ben Mbarek, mmoja wa wakosoaji wakuu wa Rais Kais Saied.
Awali kiongozi wa harakati ya Ennahda, Rached Ghannouchi, alilaani kampeni ya serikali ya Rais Kais Saied ya kuendelea kuwatiwa mbaroni wanasiasa wa upinzani na kusema kuwa, kukamatwa huko hakutatui matatizo ya wananchi.