Algeria: Mapatano ya Iran na Saudi Arabia yataimarisha usalama katika eneo
(last modified Tue, 21 Mar 2023 09:53:52 GMT )
Mar 21, 2023 09:53 UTC
  • Algeria: Mapatano ya Iran na Saudi Arabia yataimarisha usalama katika eneo

Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria ilitangaza Jumatatu usiku kwamba makubaliano yaliyotiwa saini kati ya Saudi Arabia na Iran yatasaidia kuimarisha usalama katika eneo na pia kutetea kadhia ya Palestina.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria kuhusiana na suala hilo imechapishwa baada ya Ammar Belani, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo kukutana na kufanya mazungumzo mjini Algiers na Abdallah Al-Nussiri, balozi wa Saudi Arabia nchini Algeria.

Katika kikao na balozi wa Saudi Arabia, Belani amekaribisha uamuzi wa Riyadh na Tehran wa kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati yao.

Ameongeza kuwa hatua hiyo chanya itaimarisha usalama na uthabiti katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) na kuongeza uwezo wa nchi za Kiarabu na Kiislamu kujibu kwa pamoja na kwa ufanisi changamoto na kutetea maslahi muhimu ya Umma wa Kiislamu, muhimu zaidi ikiwa ni kushughulikia matatizo na mahitaji ya watu wa Palestina.

Wakati wa mazungumzo kati ya Iran na Saudi Arabia mjini Beijing China, nchi hizo mbili zilikubaliana Ijumaa, Machi 10, kurejesha uhusiano wao wa kidiplomasia baada ya kupita miaka 7.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Saudi Arabia watakutana katika muda usiozidi miezi miwili, ili kutoa maelekezo na miongozo ya kubadilishana mabalozi na kufunguliwa tena balozi zao, pamoja na mahitaji mengine ya kuanzishwa upya mahusiano yao ya kidiplomasia.

Tangazo la makubaliano ya kurejesha uhusiano kati ya Iran na Saudi Arabia kwa upatanishi wa China na ambalo limekaribishwa na kuungwa mkono na nchi za eneo, limewatia wasiwasi mkubwa viongozi wa utawala wa Kizayuni. Wakati huo huo tangazo hilo limepokelewa shingo upande na watawala wa Marekani ambao wamesema huenda likapunguza mivutano katika eneo la Asia Magharibi na kusaidia kumaliza vita huko Yemen.

Tags