Mafuriko yaua watu 14 Somalia; madaraja, barabara na nyumba zasombwa
(last modified Tue, 28 Mar 2023 07:36:17 GMT )
Mar 28, 2023 07:36 UTC
  • Mafuriko yaua watu 14 Somalia; madaraja, barabara na nyumba zasombwa

Kwa akali watu 14 wamefariki dunia kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kusini mwa Somalia.

Mkuu wa Wilaya, Mohamed Weli Yusuf amewaambia waandishi wa habari kuwa, watu 14 wakiwemo watatu wa familia moja wameaga dunia kutokana na mafuriko hayo katika mji wa Baardhere jimbo la Jubaland kusini mwa nchi.

Ahmed Omar, mkazi wa Baardhere amesema mvua hizo zimenyesha mfululizo katika kipindi cha siku tatu zilizopita. Madaraja na barabara pamoja na mifumo mingine ya mawasiliano imehabiriwa na mafuriko hayo.

Aidha watu kadhaa wameachwa bila makazi baada ya nyumba zao kusombwa na maji ya mafuriko. Rais wa eneo la Jubaland, Ahmed Mohamed Islam ametoa mkono wa pole kwa wahanga wa janga hilo la kimaumbile.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imeonya kuhusu hatari ya kuongezeka magonjwa kama vile kipindupindu huko nchini Somalia kutokana na mafuriko hayo.

Athari za mafuriko Somalia

Mvua hizo zinanyesha nchini Somalia katika hali ambayo, ukame ambao ni mrefu zaidi kuwahi kurekodiwa katika nchi hiyo ya Pemba ya Afrika, umesababisha makumi ya maelfu ya watu kupoteza maisha.

Somalia imekabiliwa na misimu mitano mfululizo ya kutonyesha mvua, jambo ambalo limewafanya Wasomali milioni tano kukabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula, huku watoto milioni mbili wakikodolewa macho na utapiamlo.