Waliofariki dunia kwa Kimbunga Freddy Malawi wakaribia 700
Idadi ya watu walioaga dunia kutokana na Kimbunga Freddy nchini Malawi, ambacho kinatajwa kuwa kimbunga kilichodumu kwa muda mrefu zaidi, imeonezeka na kufikia watu 676.
Hayo yalisemwa jana na Charles Kalemba, Kamishna wa Idara ya Kukabiliana na Majanga nchini Malawi na kuongeza kuwa, watu wengine 1,400 wamejeruhiwa, mbali na watu 500,000 kulazimika kuishi makimbini kama wakimbizi baada ya nyumba zao kuharibiwa na kimbunga hicho.
Kalemba ameongeza kuwa, "Watu takriban 537 wangali wametoweka na hatima yao haijukulani mpaka sasa. Ni muhali kwamba wapo hai popote walipo hivi sasa, kwa kuwa zimepita siku 17 tangu watoweke."
Wakazi wanasema mamia ya watu waliofariki dunia kutokana na janga hilo la kimaumbile wamezikwa kwenye matope na hivyo huenda idadi ya waliopoteza maisha ikaongezeka hata zaidi siku zijazo.
Kimbunga Freddy kiliibuka mapema Februari kwenye pwani ya Australia na kimedumu hadi sasa na hivyo kutangazwa kuwa kimbunga kilichodumu kwa muda mrefu zaidi duniani. Kimbunga hicho kilivuka zaidi ya kilomita 8,000 kutoka mashariki hadi magharibi katika Bahari ya Hindi.

Kilitua kwa mara ya kwanza kwenye pwani ya mashariki ya Madagascar tarehe 21 Februari, na kuua watu saba. Kimbunga hicho kililifika Msumbiji na kuua watu 10 tu hapo mwanzoni mwa kutua kwake.
Kimbunga Freddy kiliikumba Madagascar kwa mara ya pili mwanzoni mwa Machi, na kuua watu wengine 10 na kisha kuhamia Msumbiji, ambako kiliua watu wengine 63.
Lakini ni nchini Malawi, ambayo haina pwani, iliyoathiriwa vibaya zaidi na kimbunga hicho ambacho kimeandamana na mvua kubwa zilizosababisha mafuruko na maporomoko ya ardhi.