Mwanaharakati wa Misri akamatwa Saudia akifanya Umra
Vyombo vya usalama vya Saudi Arabia vimeripotiwa kumtia mbaroni mwanaharakati mashuhuri wa Misri, akifanya ibada ya Umra katika mji mtukufu wa Makka.
Watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekosoa kitendo cha kutiwa mbaroni mwaharakati huyo kwa jina Rania al-Assal, ambaye alienda Saudia siku 50 zilizopita kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Umra.
Mwanahabari huyo wa kike mtajika wa Misri alitoweka asijulikane aliko tangu aliposafiri kwenda Saudi Arabia kwa ajili ya ibada hiyo ambayo pia inafahamika kama Hajj Ndogo.
Assal amekuwa muungaji mkono mkubwa wa kambi ya muqawama, sambamba na kutangaza wazi wazi kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina na Yemen. Kadhalika amekuwa akikosoa bila woga sera za Riyadh na Tel Aviv katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) kwa miaka mingi sasa.
Watumiaji wa mitandao wa kijamii na wanaharakati za kutetea haki za binadamu wamesema wanatiwa wasi wasi na kitendo hicho cha kukamatwa kwa mwandishi huyo wa habari mkosoaji wa sera za Aal-Saud hasa dhidi ya Wayemen.
Februari mwaka huu pia, watawala wa Saudia walimtia mbaroni mwanamke wa Yemen, Marwa al-Sabri, akitekeleza ibada ya Umra katika Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu mjini Makka.
Kamati ya Taifa ya Wanawake ya Yemen ililaani kitendo hicho cha kukanyagwa haki na thamani za kidini, kiutu na kimaadili za mwanamke huyo wa Kiyemen.