Sudan yalalamikia hatua ya UN kuongeza muda wa UNAMID
(last modified Mon, 20 Jun 2016 07:02:06 GMT )
Jun 20, 2016 07:02 UTC
  • Sudan yalalamikia hatua ya UN kuongeza muda wa UNAMID

Sudan imemuita mkuu wa vikosi vya kimataifa vya kusimamia amani huko Daruf UNAMID, kulalamikia hatua ya kuongezewa muda wa kuhudumu vikosi hivyo vyenye askari 20,000 kutoka nchi 30 duniani.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Sudan imemuita Martin Uhomoibh, Mkuu wa UNAMID siku chache baada ya Umoja wa Mataifa kupendekeza kuongezewa muda wa mwaka mmoja askari hao wa kulinda amani, licha ya pingamizi kutoka serikali ya Khartoum. Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imekanusha ripoti ya hivi karibuni ya UN iliyodai kuwa hali ya mambo katika jimbo la Darfur sio shwari na kwamba kuna udharura wa kuongezewa muda vikosi hivyo vya kusimamia amani. Ripoti ya pamoja ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika AU na Umoja wa Mataifa ilitoa wito wa kuviongezea vikosi hivyo vya kimataifa vya kusimamia amani muda mwingine wa mwaka mmoja, kuanzia mwishoni mwa mwezi huu hadi Juni 30 mwaka ujao wa 2017. Haya yanajiri mwezi mmoja baada ya serikali ya Khartoum kukataa kurefusha kibali cha kumruhusu Ivo Freijsen, Mkuu wa Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA kuhudumu nchini humo baada ya muda wa leseni yake kutamatika hapo Juni 6, kwa tuhuma za kuandaa kile kilichotajwa na Sudan kuwa ripoti bandia kuhusu hali ya kiusalama katika eneo la Darfur. Vikosi vya pamoja vya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa UNAMID vilitumwa huko Darfur mwaka 2007 kwa lengo la kulinda raia na kurudisha utulivu katika eneo hilo. Umoja wa Mataifa unakisia kuwa zaidi ya watu laki tatu wamepoteza maisha na wengine milioni mbili na laki 6 wakilazimika kuwa wakimbizi kutokana na machafuko ya karibu miaka 13 sasa katika jimbo hilo.