Watunisia watangaza mshikamano na waliowekwa kizuizini kwa sababu za kisiasa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i96848-watunisia_watangaza_mshikamano_na_waliowekwa_kizuizini_kwa_sababu_za_kisiasa
Vuguvugu la Uokovu wa Taifa la Tunisia limefanya mkusanyiko kwenye barabara ya Habib Bourguiba mjini Tunis kutangaza mshikamano na viongozi na wanaharakati waliowekwa kizuizini kwa sababu za kisiasa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 01, 2023 01:49 UTC
  • Watunisia watangaza mshikamano na waliowekwa kizuizini kwa sababu za kisiasa

Vuguvugu la Uokovu wa Taifa la Tunisia limefanya mkusanyiko kwenye barabara ya Habib Bourguiba mjini Tunis kutangaza mshikamano na viongozi na wanaharakati waliowekwa kizuizini kwa sababu za kisiasa.

Washiriki wa mkusanyiko huo wamesikika wakitoa nara kama "Uhuru, Uhuru... Utawala wa Kipolisi Umefikia Tamati", "Mapinduzi Yapinduliwe".
Samira Al-Shawashi, mwanachama mwandamizi wa Vuguvugu la Uokovu wa Taifa nchini Tunisia amesema pembeni ya maandamano hayo yaliyofanyika jana: "leo Rashed Al-Ghannoushi, kiongozi wa Harakati ya An-Nahdha amekuwa miongoni mwa waliowekwa kizuizini. Alikamatwa kwa kutoa maoni yake na ameshtakiwa kwa sababu alijaribu kuchukua hatua kuelekea umoja wa kitaifa".
Al-Shawashi ameongezea kwa kusema: "wale wote waliowekwa kizuizini kwa tuhuma za kula "njama dhidi ya usalama wa serikali" kwa kweli wako mbali kabisa na njama yoyote dhidi ya usalama wa serikali.
Rashed Al-Ghannoushi

Mwanachama huyo wa Vuguvugu la Uokovu wa Taifa nchini Tunisia amesisitiza kwa kusema: "Vuguvugu la Uokovu wa Taifa na makundi yote ya kupigania demokrasia ambayo yamehudhuria mkusanyiko huu ​​hayataacha matakwa yao ya kupatikana umoja wa kitaifa".

Kabla ya hapo Rashid Al-Ghannoushi alitangaza kuwa, kukamatwa kwake kwa tuhuma za kula njama dhidi ya usalama wa nchi ni hatua ya kisiasa.
Mbali na Rashid al-Ghannoushi, ambaye ni kiongozi wa chama cha upinzani chenye mielekeo ya Kiislamu cha An-Nahdhah, mahakama ya Tunisia imetoa waranti wa kukamatwa Youssef al-Nuri, Ahmed al-Mashreghi, Rafiq Abdessalam na wanachama wengine kadhaa wa chama hicho. Al-Ghannoushi amesema, kukamatwa na kushtakiwa wanachama wote hao wa An-Nahdhah ni kwa sababu za kisiasa tu.
Siku ya Alkhamisi iliyopita, tovuti ya Al-Sharooq ya Tunisia iliripoti kuwa Rashed Al-Ghannoushi alitiwa gerezani baada ya kusailiwa kwa muda wa masaa tisa.../