May 07, 2023 11:01 UTC
  • Vyama 20 vyalitaka Baraza la Kijeshi linalotawala Mali kutupilia mbali mpango wa kuondoa dini katika rasimu ya katiba

Takriban vyama 20 nchini Mali vimeunganisha pamoja juhudi zao na kulitaka baraza tawala la kijeshi kufuta kipengee kwenye rasimu ya katiba mpya kinachosisitiza kuwa serikali ya nchi hiyo itakuwa ya kilaiki. Rasimu hiyo imepangwa kupigwa kura ya maoni mwezi ujao wa Juni.

Vyama hivi vya kidini, kitamaduni na kisiasa vimemtaka mkuu wa serikali ya kijeshi, Kanali Asimi Guetta, kuanzisha mashauriano kwa lengo la kutupilia mbali kipengee hicho kwenye rasimu ya katiba mpya ya Mali.

Vyama hivyo vimetahadharisha kwamba, iwapo hilo halitafanikiwa, vitaanzisha kampeni ya kupiga kura ya kuikataa rasimu ya katiba katika kura ya maoni itakayofanyika Juni 18.

Taarifa ilitotolewa na vyama hivyo imesema, kamati iliyopewa jukumu la kupitia  rasimu ya katiba ilipaswa kuikomboa Mali kutoka kwenye "kizuizi cha itikadi iliyorithiwa kutoka kwa Ufaransa", lakini imekosa "ujasiri".

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Licha ya madhara yake kwa nchi yetu tangu baada ya kupata uhuru hadi leo, lakini kifungu kinachosema kuwa serikali ya Mali ni ya kilaiki kimeendelea kuwapo na kutajwa kuwa hakipingani na itikadi za kidini."

Ufaransa imedumisha ushawishi wake wa kisiasa na kijeshi nchini Mali katika miongo kadhaa iliyopita, lakini mnamo Agosti 15, 2022 ilitangaza kuondoa vikosi vyake vya mwisho vya kijeshi nchini humo.

Kura ya maoni kuhusu katiba mpya ni hatua ya kwanza katika mchakato ulioainishwa na baraza la kijeshi, kuelekea uchaguzi wa Februari 2024 kwa lengo la kurejesha madarakani utawala wa kiraia.

Tags