Arab League yatoa rasimu ya mpango wa kutatua mzozo wa Sudan
Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) wametayarisha rasimu ya mpango wa kutatua mgogoro wa Sudan.
Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wametangaza rasimu ya mpango huo katika mkutano wao uliofanyika leo Jumapili mjini Cairo, ambao lengo lake ni kutatua kabisa mgogoro wa Sudan, wakisisitiza haja ya kuheshimiwa mamlaka ya kitaifa na ukamilifu wa ardhi ya nchi hiyo.
Katika rasimu hiyo, mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wanataka kufikiwa usitishaji vita kamili na wa kudumu nchini Sudan kwa kukomesha uingiliaji wowote wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo, na pia kubuni njia ya mawasiliano kati ya pande mbili zinazozozana ili kuingia katika awamu ya utekelezaji wa maamuzi ya kutatua mgogoro wa sasa katika nchi hiyo ya Afrika.
Licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Sudan, vita vinaendelea katika maeneo mbalimbalii ya nchi hiyo, na hadi sasa mamia ya watu wameripotiwa kuuawa na maelfu kujeruhiwa.
Ripoti zinasema, watu waliolazimika kukimbia makazi yao kutokana na mapigano wameachwa njia panda na hawana chaguo jingine isipokuwa kurejea katika vitongoji vyenye usalama mdogo vya mji mkuu, Khartoum, kwa ajili ya kutafuta mkate na mahitaji mengine.
Hospitali nyingi za Sudan zinashindwa kutoa huduma kwa sababu ya uhaba wa dawa. Kwa mujibu wa Muungano wa Madaktari wa Sudan, wafanyikazi wa masuala ya tiba hawawezi kufika mahospitalini huku vituo mbalimbali vya afya vikiwa vimeharibiwa au kutekwa na kugeuzwa kambi za kijeshi.
Mapigano makali yalizuka Aprili 15 kati ya kiongozi mkuu wa Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye anaongoza jeshi la kawaida, na naibu wake aliyegeuka mpinzani Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, ambaye anaongoza Kikosi cha Radiamali ya Haraka (RSF).