Wanachama 14 wa Ikhwanul-Muslimin ya Misri wahukumiwa kifungo cha maisha jela
May 22, 2023 09:26 UTC
Mahakama moja nchini Misri, imemhukumu Hamza Zouba, mkuu wa kamati ya habari ya Harakati ya Ikhwanul-Muslimin na wajumbe 13 wa kamati hiyo kifungo cha maisha jela, sambamba na kutoa hukumu ya kifungo cha miaka 15 jela kwa wanachama wengine watatu wa harakati hiyo ya Kiislamu.
Katika miaka ya hivi karibuni, vyombo vya mahakama vya Misri ambavyo vina mfungamano na serikali ya rais wa nchi hiyo Abdel Fattah al-Sisi, imewahukumu adhabu ya kifo wanachama wengi wa Ikhwanul Muslimin au vifungo vya muda mrefu jela kwa makosa bandia.
Katika miaka michache iliyopita, wanachama wengi wa harakati hiyo wamekamatwa na kufungwa jela na baadhi ya viongozi wake wamefia gerezani au wakati wa kesi zao zinasikilizwa mahakamani.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, mahakama ya Misri imedai kuwa watu hao 14 wanatuhumiwa kujiunga na kundi la kigaidi, kueneza habari za uongo zinazovuruga usalama wa umma na kuyafadhili kifedha makundi ya kigaidi.
Serikali ya Misri imeitangaza harakati ya Ikhwanul-Muslimin kuwa ni kundi la kigaidi na ilipiga marufuku shughuli za harakati hiyo kongwe ya Kiislamu baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa madarakani serikali halali ya hayati Muhammad Morsi.
Itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Julai 2013, Abdel Fattah al-Sisi akiwa mkuu wa majeshi ya Misri wakati huo, alimuondoa madarakani Mohammad Morsi kupitia mapinduzi ya kijeshi.
Tangu aingie madarakani kama rais wa nchi mnamo mwaka 2014, al-Sisi amekuwa akitekeleza sera ya kukandamiza upinzani kwa uungaji mkono wa nchi za Magharibi.
Mashirika mengi ya kimataifa na ya kutetea haki za binadamu yametahadharisha kuhusiana na utendaji wa Abdel Fattah al-Sisi katika uga wa uhuru wa kijamii na kisiasa na ukiukaji wa haki za binadamu nchini Misri.../
Tags