MSF: 180 wamepoteza maisha katika kambi ya wakimbizi Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i9784-msf_180_wamepoteza_maisha_katika_kambi_ya_wakimbizi_nigeria
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka MSF limesema makumi ya watu wamepoteza maisha kutokana na mkurupuko wa ugonjwa wa kuendesha na kutapika katika kambi moja ya wakimbizi nchini Nigeria, katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 23, 2016 03:30 UTC
  • MSF: 180 wamepoteza maisha katika kambi ya wakimbizi Nigeria

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka MSF limesema makumi ya watu wamepoteza maisha kutokana na mkurupuko wa ugonjwa wa kuendesha na kutapika katika kambi moja ya wakimbizi nchini Nigeria, katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.

Taarifa ya shirika hilo imesema watu 188 wameaga dunia kutokana na ugonjwa wa kuendesha, kutapika na kuishiwa maji mwilini wakiwa katika kambi ya wakimbizi ya Bama, iliyoko katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Taarifa hiyo ya MSF imeongeza kuwa, watoto 800 wanakabiliwa na utapiamlo katika kambi hiyo, huku 16 miongoni mwao wakiwa katika hali mahututi na kwamba kwa sasa wanapokoea huduma za matibabu katika zahanati moja katika eneo la Maiduguri.

Mwezi Machi mwaka huu, Benki ya Dunia ilisema wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram nchini Nigeria hadi sasa wameua watu zaidi ya 20 elfu na kusababisha hasara ya dola bilioni 5.9 katika jimbo la Borno. Aidha ripoti hiyo ilisema zaidi ya watu milioni mbili wamefanywa wakimbizi kufuatia ugaidi wa Boko Haram.