Somalia kuanzisha upigaji kura wa moja kwa moja wa wananchi mwaka 2024
Somalia imetangaza kuwa itaanzisha mfumo wa upigaji kura wa moja kwa moja wa wananchi. Hatua hii inafuatia ahadi ya Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia mwezi Machi mwaka huu ya kukomesha mfumo tata wa upigaji kura usio wa moja kwa moja unaoendelea tangu mwaka 1969.
Imeelezwa kuwa "Kanuni za kimsingi zinapaswa kuwa kwamba uchaguzi wa Shirikisho la Jamhuri ya Somalia lazima uwe ule unaowapa umma fursa ya kupiga kura zao kidemokrasia katika mfumo wa mtu mmoja, wa kura moja." Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na serikali ya Somalia baada ya kufikia makubaliano na viongozi wa majimbo ya nchi hiyo.
Taarifa ya pamoja ya pande mbili hizo imeongeza kuwa, mageuzi haya yamekusudiwa ili kushajiisha mfumo wa kisiasa wa vyama vingi.
Somalia inapambana kujinasua katika miongo kadhaa ya machafuko na ukosefu wa amani unaosababishwa na hujuma na mashambulizi ya kundi la wanamgambo wa al Shabaab, huku nchi hiyo ikifanya juhudi za kukabiliana na athari mbaya za majanga ya kimaumbile kama ukame mkubwa ulioikumba nchi hiyo na kusababishia njaa ya mamilioni ya watu.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, Somalia haijawahi kuwa na uchaguzi wa mtu mmoja, kura moja tangu mwaka 1969 wakati dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Siad Barre alipotwaa madaraka. Badala yake koo za nchi hiyo ndizo zimekuwa zikichukua maamuzi na kupanga sera za nchi huku majukumu yenye ushawishi kama vile Spika wa Bunge, Waziri Mkuu na Rais yakigawanywa miongoni mwa makundi yenye ushawishi nchini humo. Vilevile mabunge ya majimbo na wajumbe wa koo ndiyo yanayochagua wabunge wa Bunge la Taifa ambao nao humchagua Rais wa nchi.
Hata hivyo upinzani kati ya koo mbalimbali umepelekea kushuhudiwa hitilafu na mizozo ya kisasa kwa miongo kadhaa, ambayo katika miaka ya hivi karibuni imetumiwa vibaya na wanamgambo wa Al-Shabaab wenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa la Al-Qaeda.