May 31, 2023 11:32 UTC
  • Umoja wa Afrika: Tunapinga uingiliaji wa kigeni katika masuala ya Sudan

Umoja wa Afrika umesisitiza kuwa, unapinga uingiliaji wa kigeni katika masuala ya Sudan na kwamba, hilo ni jambo lisilokubalika.

Taarifa ya Umoja wa Afrika imeeleza kuwa, umoja huo hautakubaliana na vitendo vyovyote vile vya kutaka kuingilia masuala ya ndani ya Sudan ambayo kwa sasa inasumbuliwa na vita vya ndani.

Umoja wa Afrika umesisitiza pia katika sehemu nyingine ya taarifa yake hiyo kwamba, mgogoro wa sasa wa Sudan hauwezi kupatiwa ufumbuzi kwa mtutu wa bunduki.

Taarifa ya Umoja wa Afrika inatolewa katika hali ambayo, mapigano nchini Sudan yameendelea kushuhudiwa licha ya kutolewa miito ya kusitisha mapigano na hata kufikiwa makubaliano ya usitishaji vita.

Wakati huo huo maafisa wa Sudan wanasema jeshi la nchi hiyo limesitisha mazungumzo ya kusimamisha mapigano na wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF), wakilishutumu kundi hilo kuwa limekuwa likikiuka mara kwa mara makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano.

Abdel Fattah al-Burhan

Afisa wa serikali ya Sudan ambaye hakutaja jina lake litajwe ameviambia vyombo vya habari kwamba, jeshi limechukua uamuzi huo "kwa sababu waasi hawajawahi kutekeleza hata moja ya vipengee vya usitishaji vita wa muda mfupi, na wamekiuka makubaliano mara kwa mara ."

Hivi majuzi Umoja wa Afrika (AU) ulipasisha Mwongozo wa Utatuzi wa Mzozo nchini Sudan unaolenga kukomesha sauti za bunduki na kurejesha usalama wa kudumu nchini Sudan.

Mpango huo una vipengele sita ambavyo ni pamoja na kuanzishwa utaratibu wa kuwa na mawasiliano ya karibu na pande hasimu ili kuhakikisha juhudi zote za kikanda na kimataifa zinawiana na kuwa na matokeo mazuri; kukomesha mzozo mara moja, kurejesha amani ya kudumu kwa kujumuishwa pande zote na kufikishwa vizuri misaada ya kibinadamu.

Tags