Jun 03, 2023 01:33 UTC

Mwanaharakati mmoja wa kisiasa amesema kadhia ya Sahara Magharibi haijapatiwa ufumbuzi kwa muda mrefu sasa kutokana na unafiki wa nchi za Magharibi.

Talen Ali Salem ameliambia shirika la habari la Russia Today kuwa, mzozo wa eneo la Sahara Magharibi ungelikuwa umepatiwa ufumbuzi iwapo Wamagharibi wangelikuwa na azma na irada ya kisiasa ya kuushughulikia.

Kwa mujibu wa mwanaharakati na mchambuzi huyo wa kisiasa, "Morocco ni muitifaki mkuu wa NATO na nchi za Magharibi huko kaskazini mwa Afrika, na Sahara Magharibi ni koloni lao la mwisho la barani Afrika."

Morocco inaliangalia eneo la Sahara Magharibi, ambalo ni koloni la zamani la Uhispania, kuwa ni eneo lililo chini ya mamlaka yake, wakati jirani yake Algeria inaiunga mkono na kuipa hifadhi Harakati ya Polisario inayopigania ukombozi na kujitawala kwa eneo hilo tokea miaka ya 70.

Vita vya kupigania uhuru baina ya harakati ya Polisario na Morocco vilianza mwaka 1975 na  kuendelea hadi mwaka 1991 na kisha pande mbili zilisitisha mapigano kwa upatanishi wa Umoja wa Mataifa.

Wanaharakati wa Polisario

Talen Ali Salem ameiambia Russia Today kuwa, hali ya Sahara Magharibi ni mfano wa wazi wa unafiki wa nchi za Magharibi, ambazo kwa upande mmoja zinadai kuheshimu 'nidhamu ya dunia' na haki za binadamu, na kwa upande mwingine haziheshimu uhalali wa Sahara Magharibi.

Kwa sasa, Morocco inadhibitii asilimia 80 ya eneo la Sahara Magharibi huku sehemu iliyosalia ikishikiliwa na Harakati ya Polisario inayoungwa mkono na Algeria. Kwa zaidi ya miaka 15, Polisario imepigana vita na Morocco vya kulikomboa eneo hilo, baada ya Uhispania kuondoa askari wake mwaka 1975 na inataka iitishwe kura ya maoni ya kuamua uhuru na kujitawala watu wa Sahara Magharibi

Tags