Mazungumzo ya simu ya Marais Kenyatta na Obama
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i9841-mazungumzo_ya_simu_ya_marais_kenyatta_na_obama
Rais Barack Obama wa Marekani amefanya mazungumzo na mwenzake wa Kenya Uhuru Kenyatta kuhusu masuala ya uhusiano wa pande mbili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 24, 2016 03:41 UTC
  • Mazungumzo ya simu ya Marais  Kenyatta na Obama

Rais Barack Obama wa Marekani amefanya mazungumzo na mwenzake wa Kenya Uhuru Kenyatta kuhusu masuala ya uhusiano wa pande mbili.

Imearifiwa kuwa, katika mazungumzo hayo ya Alhamisi, wawili hao wamezungumza kuhusu masuala kama vile, mapambano na ugaidi na hatua ilizopiga Kenya katika kurejesha usalama. Katika mazungumzo hayo, Rais Kenyatta amebainisha wazi changamoto inazokumbana nazo Kenya katika kuwapa hifadhi maelfu ya wakimbizi katika miongo miwili iliyopita na kwa msingi huo ametaka jamii ya kimataifa iunge mkono nchi yake katika suala hilo. Kenyatta aidha amemfahamisha Obama kuwa, Kenya itatekeleza majukumu yake ya kimataifa kuhusu kulinda usalama na hadhi ya wakimbizi. Obama ameahidi kuisaidia Kenya kuwahudumia wakimbizi na jamii ambazo zinawapokea wakimbizi nchini humo.

Kenya iko chini ya mashinikizo ya kimataifa kubatilisha uamuzi wake wa kufunga kambi ya Daadab yenye wakimbizi takribani 330,000 na hivyo kuifanya kuwa kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani. Kambi hiyo yenye wakimbizi Wasomali iko eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya. Serikali ya Kenya inasema kambi hiyo inatumika kutoa mafunzo kwa magaidi wa al Shabab wanaotekeleza hujuma nchini humo. Aidha serikali ya Kenya inasema wakimbizi hao wanaisababishia nchi hiyo matatizo ya kifedha na kimazingira.