UN: Mapigano yasimamishwe mara moja nchini Somalia
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa wito kwa pande zinazozozana kutia saini makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Somalia likisisitiza udharura wa kuheshimiwa kikamilifu mamlaka, uhuru wa kisiasa na umoja wa ardhi ya Somalia.
Katika kikao chao cha jana, wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa walielezea wasiwasi wao kuhusu ghasia zinazoendelea huko Las Anod katika mkoa wa Sool, kaskazini mwa Somalia, ambazo zimesababisha vifo vya raia wengi na kulazimisha zaidi ya watu 150,000 kuhama makazi yao.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia limetaka kuwepo mazungumzo jumuishi na utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani.
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani vikali mapigano makali kati ya vikosi vya usalama vya Somaliland na makundi ya wanamgambo na vitendo vyote vya unyanyasaji dhidi ya raia na uharibifu wa miundombinu ya raia unaosababishwa na mapigano hayo.
Baraza la Usalama pia limetoa wito wa kurudi nyuma mara moja kwa vikosi vya usalama vya "Somaliland" na limezitaka pande zote kujiepusha na uchochezi na uhamasishaji wa vitendo vya ukatili ili kupunguza mivutano na kurejesha hali ya kuaminiana.