Magaidi 19 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab waangamizwa Somalia
Wanachama wasiopungua 19 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wameangamizwa kufuatia operesheni ya jeshi la Somalia katika eneo la kusini la Lower Shabelle.
Vyombo vya usalama vya Somalia vimethibitisha kuuawa wanachama hao wa kundi la kigaidi na kueleza kwamba, operesheni hiyo imeongozwa na Idara ya Taifa ya Intelijensia na Usalama ya Somalia (NISA).
Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu, operesheni hiyo imefanyika katika kijiji cha Bula-Mohamed-Abdalla, viungani mwa mji wa Awdheegle, katika jimbo la Lower Shabelle.
Habari zaidi zinasema kuwa, magari na silaha za magaidi hao zimeharibiwa kwenye operesheni hiyo katika mji huo wa kilimo unaopatikana yapata kilomita 84 magharibi mwa Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.
Operesheni hiyo imejiri siku chache baada ya askari 54 wa Jeshi la Ulinzi la Uganda UPDF wanaohudumu chini ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) kuuawa katika shambulio la al-Shabaab katika mji wa Bulo-Mareer, umbali wa kilomita 110 kusini mwa Mogadishu.
Haya yanajiri siku chache baada ya jeshi la Somalia kufanikiwa kuzima shambulizi la wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab katika Mkahawa wa Perls, kwenye fukwe za Bahari Hindi. Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, watu tisa waliuawa katika shambulizi hilo.
Vikosi vya serikali ya Somalia vikisaidiwa na wapiganaji wa kieneo waliochoshwa na jinai za genge la ukufurishaji la al-Shabab vimezidisha mashambulizi dhidi ya magaidi hao ambao wamedai kuhusika na mfululizo wa mashambulio ya kigaidi ndani na nje ya Somalia.