Kuendelea mgogoro wa Tunisia; kifungo cha maisha kwa Rashid al-Ghannouchi
(last modified Tue, 13 Jun 2023 02:17:23 GMT )
Jun 13, 2023 02:17 UTC
  • Kuendelea mgogoro wa Tunisia; kifungo cha maisha kwa Rashid al-Ghannouchi

Baada ya kupita miezi miwili tangu atiwe mbaroni, Rashid al-Ghannouchi, Kiongozi wa Harakati ya al-Nahdha ya Tunisia, mahakama ya mwanzo wa mji wa Ariana imemhukumu mwanasiasa huyo mashuhuri kifungo cha maisha jela.

Al-Ghannouchi, mwenye umri wa miaka 81 ambaye alikuwa spika wa bunge la Tunisia kabla ya kuvunjwa na Rais Saied mnamo Julai 2021, alikamatwa tareje 17 mwezi wa Aprili mwaka huu (2023) na tangu wakati huo amekuwa akishikiliwa kizuizini kwa tuhuma za kupanga njama dhidi ya usalama wa nchi.

Kukamatwa kwa kiongozi wa harakati ya al-Nnahdha ya Tunisia kulifanyika kufuatia kushadidi mgogoro wa kisiasa na kiuchumi nchini humo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Spika huyo wa zamani wa bunge la Tunisia ni miongoni mwa zaidi ya wapinzani 20 wa kisiasa wa Kais Saied, wakiwemo mawaziri wa zamani na wafanyabiashara waliokamatwa tangu mwezi Februari mwaka huu.

Julai 2021, Rais wa Jamhuri ya Tunisia, Kais Saied, alipiga marufuku shughuli za vyama vya siasa na kufanya mabadiliko katika katiba, suala lililochochea mzozo wa kisiasa nchini humo. Kais Saied pia allivunja Bunge la Taifa na kumfuta kazi Waziri Mkuu na hivyo kutwaa madaraka yote ya nchi, jambo ambalo limepingwa na vyama vya siasa vinavyosema hatua za kiongozi huyo ni mapinduzi dhidi ya katiba na demokrasia changa ya nchi hiyo. Hatua hizo za rais wa Tunisia zilizua makelele mengi na kuvifanya vyama na miungano ya wafanyakazi kujitokeza na kupinga hatua hizo. Chama cha al-Nahdha ambacho kinahesabiwa kuwa chama kikuu cha upinzani nchini Tunisia kilipinga vikali na kwa sauti kubwa maamuzi na hatua zilizochukuliwa na Rais wa nchi na kuzitambua kama zinazokwenda kinyume na demokrasia pamoja na malengo makuu ya wananchi wa nchi hiyo walioanzisha vuguvugu la umma lililohitimisha udikteta wa Rais Zainul-Abidin bin Ali.

Rais Kais Saied wa Tunisia

 

Mashinikizo na upinzani wa chama cha al-Nahdha ulipelekea chama hicho pamoja na kiongozi wake Rashid al-Ghannouchi kiandamwe na mashinikizo makubwa ambapo katika majuuma ya hivi karibuni makumi ya wanachama wake wamekamatwa na kusweka ndani akiwemo kiongozi wake. Katika ripoti yake ya hivi karibuni, Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetangaza kuwa, viongozi wa serikali ya Tunis wameshadidisha hujuma na kamakata zao dhidi ya wapinzani na wanachukua hatua zenye lengo la kukisambaratisha kabisa chama kikuu cha upinzani katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Salsabil Chelali, mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch nchini Tunisia anasema: Baada ya juhudi za kuitisha al-Nahdha na kutoa shutuma nzito dhidi yake bila ushahidi, maafisa wa Rais wa Tunisia, Kais Saied, wamechukua hatua ya kukisambaratisha kabisa chama hicho cha upinzani.

Pamoja na hayo, Al-Ghannouchi amekuwa akitoa mwito wa kuwepo maridhiano, umoja wa kitaifa na kuwekwa kando vitendo vya utumiaji mabavu nchini Tunisia. Chama cha al-Nahdha kimemtaka Rais wa Tunisia kufungua mazungumzo na vyama vya siasa na mashirika ya kiraia ili kuinasua nchi hiyo kutoka katika mkwamo wa kisiasa na kiuchumi unaoikabili nchi.

Nembo ya chama cha al-Nahdha

 

Chama cha al-Nahdha chenye mielekeo ya Kiislamu kimetangaza masharti kadhaa kwa ajili ya kufungua ukurasa mpya katika uhusiano wake na Rais wa nchi hiyo.

Manzer Venisi, kiongozi wa muda wa chama cha al-Nahdha, amesema kwamba chama hicho kiko tayari kufungua "ukurasa mpya" katika mahusiano yake na Rais Kais Saied, ikiwa atakubali kupitia upya mchakato wake wa kisiasa na kujiepusha kuwakamata na kuwaweka kizuizini viongozi wa upinzani.

Pamoja na hayo yote, lakini Rais Kais wa Tunisia ameendelea kutekeleza ulipizaji kisasi wa kisiasa. Hii ni katika hali ambayo, siyo tu kwamba, matunda na malengo ya wananchi ya kuhitimisha utawala wa kidikteta wa bin Ali yapo katika hatari ya kuangamia, bali matatizo ya kiuchumi yanaisakama mno nchi hiyo na yameshadidi sana na inaonekana kuwa, Watunisia watakabiliwa na hali ngumu zaidi katika siku za usoni.