Rais wa Nigeria afanya mabadiliko makubwa; apangua safu ya wakuu wa usalama
-
Rais Bola Ahmed Tinubu
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais wa Nigeria imeeleza kuwa Rais Bola Ahmed Tinubu wa nchi hiyo amewateua makamanda wapya wa vikosi vya jeshi la taifa, wanamaji na jeshi la anga.
Rais wa Nigeria Bola Tinubu amefanya mabadiliko makubwa katika vikosi vya ulinzi, na hivyo kuwastaafisha mapema wakuu wa usalama na polisi ikiwa ni chini ya mwezi mmoja tangu ashike hatamu za uongozi huko Nigeria. Tinubu aliapishwa kuwa Rais wa Nigeria Mei 29 mwaka huu.
Itakumbukwa kuwa Rais wa Nigeria amekuwa akitoa kipaumbele kikubwa kwa suala la usalama nchini humo na ameahidi kufanya mabadiliko katika sekta ya ulinzi na usalama nchini humo ikiwa ni pamoja na kuwaajiri wanajeshi na maafisa zaidi wa polisi, kuwalipa mishahara mizuri na kuwapatia suhula na vitendea kazi vilivyo bora.
Rais wa Nigeria alisema katika siku yake ya kwanza ya kuhudumu mamlakani kwamba: "Tutawekeza zaidi katika wafanyakazi wetu wa idara ya usalama, na hii ina maana ya kuongeza idadi ya wafanyakazi. Tutawapa mafunzo vifaa, na malipo bora."
Weledi wa mambo wanasema si jambo la kawaida kwa Rais kuwastaafisha mapema wakuu wa usalama mara baada ya kuingia madarakani.
Hii si mara ya kwanza kwa Rais wa Nigeria kufanya mabadiliko ya viongozi wa idara mbalimbali za serikali, kwani Alhamisi iliyopita pia Rais Tinubu Rais Bola Tinubu alimsimamisha kazi Mkuu wa Kamisheni ya Kupambana na Ufisadi ya nchi hiyo ambaye alikuwa akichunguzwa kwa tuhuma za kutumia vibaya madaraka. Abdul Rasheed Bawa alisimamishwa kazi na Rais Tinubu kutokana na tuhuma kubwa za kutumia vibaya madaraka yake.
Bawa amesimamishwa kazi wiki mbili tangu Godwin Emefiele, aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya nchi hiyo, afukuzwe kazi na kutiwa mbaroni.