Safari ya Rais Ebrahim Raisi wa Iran nchini Uganda
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Jumatano jioni aliwasili Kampala katika safari rasmi ya siku mbili nchini Uganda ikiwa ni katika duru pili ya safari yake ya kikanda katika bara la Afrika. Safari hiyo imefanyika kwa mwaliko rasmi wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda.
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Jumatano, Julai 21, alianza safari ya kuzitembelea nchi tatu za mashariki na kusini mwa bara la Afrika: Kenya, Uganda na Zimbabwe kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano na nchi za Afrika. Akiwa Nairobi alikutana na kuzungumza na Rais William Ruto wa nchi hiyo ambapo maafisa wa ngazi za juu wa nchi hizo mbili walitia saini hati 5 muhimu za ushirikiano.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inajaribu kuanzisha duru mpya ya uhusiano wake na Bara la Afrika kwa kupanua ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi. Afrika inaweza kutoa sehemu ya malighafi zinazohitajika na Iran, na Tehran kulipa bara la Afrika huduma za kiufundi na uhandisi, mashine, bidhaa, vifaa vya matibabu na dawa katika soko kubwa la Afrika.
Kiwango cha juu cha ongezeko la watu, pamoja na uwezo mkubwa wa kiuchumi na kibiashara na migodi mikubwa ya madini barani Afrika, ni mambo ambayo yamezipelekea nchi nyingi kuonyesha hamu ya kuwekeza katika bara hilo.
Baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kutokana na sera za Iran za kupanua uhusiano na nchi za Kiafrika, uhusiano na Uganda pia uliamilishwa, ambao mara nyingi ulihusishwa na ugawaji wa mikopo ya kifedha na misaada ya kiuchumi kwa nchi hii.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi zilizochapishwa, jumla ya biashara kati ya Iran na Uganda mwaka jana ilipungua kidogo ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.
Mwaka jana, Iran ilisafirisha takriban dola milioni 1.2 za bidhaa mbalimbali nchini Uganda, na kwa kuzingatia uzalishaji wa kiviwanda wa Iran na mahitaji ya Uganda kutoka nje, uchumi wa nchi hizo mbili unaweza kukamilishana katika nyanja nyingi.
Ikiwa na utajiri mkubwa wa madini kama vile shaba, kobalti, madini ya chuma, dhahabu, hifadhi ya mafuta na gesi, pamoja na udongo wenye rutuba kwa kilimo, Uganda inaweza kuwa kituo kikubwa cha uwekezaji kwa mashirika ya Iran.
Kwa upande mwingine, uanachama wa Uganda katika jumuiya muhimu za kiuchumi za kikanda kama vile Umoja wa Kiuchumi wa Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (Comesa) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Eneo la Biashara Huru Barani Afrika (AfCFTA) unatoa fursa kwa mashirika ya Iran kuweza kufika katika soko kubwa la bara Afrika.
Iran, ikiwa ni nchi yenye nguvu ya kieneo na yenye miundombinu ya usafiri wa reli na barabara na bandari muhimu za kibiashara katika Ghuba ya Uajemi, inaweza kuwa kituo cha mawasiliano kati ya Uganda na nchi za Asia ya Kati, Caucasus na Russia kwa ajili ya mauzo ya bidhaa zake kuu za kilimo, hasa chai na kahawa.

Ushirikiano katika nyanja za mafuta, dawa, huduma za kiufundi na uhandisi, zikiwemo katika sekta za ujenzi wa barabara, uzalishaji wa umeme, uvutaji maji, mabomba na usambazaji wa maji ya kunywa, na kutoa mbinu mpya za kuboresha umwagiliaji katika ardhi yenye rutuba ya Uganda ni maeneo mengine yanayofaa kwa ajili ya ushirikiano wa pamoja kati ya Iran na Uganda.
Kwa hivyo, ziara ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Uganda na kufikiwa mikataba mipya kunaweza kutoa misingi muhimu ya kupanuliwa uhusiano wa nchi mbili hizi.