Aug 04, 2024 07:24 UTC

Duru za habari za utawala wa Kizayuni wa Israel zimetangaza kuwa, ving'ora vilisikika mtawalia jana, kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, kutokana na mashambulizi makali yaliyofanywa na Hizbullah ya Lebanon.

Kwa mujibu wa tovuti ya televisheni ya al-Masirah, vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vilitangaza jana Jumamosi kwamba ving'ora hivyo vya hatari vimesikika vikilia mfululizo katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Aljalil (Galilaya) Magharibi kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Wakati huo huo, muqawama wa Kiislamu wa Lebanon umetangaza kuwa umekishamnbulia vikali na kituo kimoja cha Wazayuni na kukisababishia hasara kubwa. 

Idara ya Habari za Kivita ya Hizbullah ya Lebanon imetangaza kuwa, ikiwa ni katika kuliunga mkono taifa lenye msimamo thabiti la Palestina huko Ghaza na katika kukabiliana na mashambulizi ya adui Mzayuni kwenye vijiji visivyotetereka vya kusini mwa Lebanon, wanamapambano wa kambi ya Muqawama wa Kiislamu, wameendelea kumtia hasara adui kwa kushambulia kwa wimbi la makombora, maeneo ya adui huyo.

Tangu ilipofanyika operesheni ya kishujaa ya Kimbunga cha al Aqsa iliyoongozwa na HAMAS na kuifedhehesha vibaya Israel, harakati nyingine za muqawama ikiwemo Hizbullah ya Lebanon zimeingia vitani kuwasaidia ndugu zao Wapalestina na zimekuwa zikiusababishia hasara kubwa utawala wa Kizayuni licha ya harakati hizo kutoa muhanga watu wake na makamanda wake mbalimbali kwenye vita hivyo vya Jihadi. 

Tags