Ulimwengu wa Michezo, Agosti 26
Hujambo mpenzi msikilizaji na hususan shabiki na mfuatiliaji wa habari za spoti. Karibu tuangazie baadhi ya matukio makubwa ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita kitaifa na kimataifa….
Iran bingwa wa mieleka
Kwa mara nyingine tena, timu ya taifa ya Iran ya mieleka ya vijana mtindo wa Greco-Roman imetwaa ubingwa wa dunia baada ya kuzoa medali sita katika Mashindano ya Dunia ya Vijana wenye chini ya miaka 17 ya 2024 huko Amman, mji mkuu wa Jordan. Kwenye mashindano hayo yaliyomalizika Agosti 25, timu ya Iran ilitetea taji la ubingwa na kuibuka kidedea tena kwa kuzoa medali 3 za dhahabu na 3 za shaba. Armin Shamsipour, Amir Mahdi Saeidi Nava, na Danial Izadi walishinda dhahabu katika kategoria za kilo 48, 65 na 92 huku, Abolfazl Karami, Emadreza Mohsen-Nejad, na Ali Asghar Dadbakhsh walitia kibindoni medali za shaba katika kategoria za kilo 51, 80 na 110 mtawalia.
Timu ya Iran ilinyakua taji la ubingwa kwa alama 140, huku Uzbekistan na Azerbaijan zikiambulia nafasi za pili na tatu kwa alama 113 na 105 mtawalia.
Klabu Bingwa Afrika
Mechi za Klabu Bingwa Barani Afrika zimeendelea kurindima, huku baadhi ya miamba ya soka katika bara hilo wakilambishwa sakafu na baadhi wakisogea mbele kwa madaha. Klabu ya Yanga ya Tanzania imefuzu kucheza raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuichabanga Vital’O ya Burundi magoli 6-0 katika mchezo wa pili wa hatua ya kwanza. Mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam Jumamosi unaifanya Yanga kufuzu kwa jumla ya magoli 10-0, kwa kuwa mchezo wa kwanza ilishinda magoli 4-0. Clatous Chama ameandika rekodi kuwa mchezaji wa kwanza CAF Champions League kutoa assists (4) katika mechi moja na kufunga bao 1. Mbali na goli la Chama la dakika ya 50 ya mchezo, mabao mengine ya Wananchi yalifungwa na Pacome Zouzoua (Penati) katika dakika ya 13, Clement Mzize dakika ya 48, Prince Dube dakika ya 71, Stephane Aziz Ki dakika ya 79, huku msumari wa mwisho ukisindiliwa jenezani na nyundo ya Mudathir Yahya kunako dakika ya 84.
Wakati huo huo, klabu ya Azam ya Tanzania imesukumizwa nje ya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kukubali kulishwa kichapo cha jumla cha mabao 2-1 na APR ya Rwanda kwenye mchezo wa hatua ya awali. APR imetinga raundi ya kwanza ambapo watachuana na Pyramids ya Misri. Mbali na Azam, klabu nyingine za Tanzania zilizoyaaga mashindano hayo ni pamoja na Coastal Union, JKU na Uhamiaji.
Huku hayo yakiarifiwa, Gor Mahia ya Kenya siku ya Jumapili ilishuka katika dimba la Nyayo jijini Nairobi kutoana udhia na Al-Merreikh Bentiu ya Sudan Kusini katika mchuano wa mkondo wa pili wa mechi za Klabu Bingwa Afrika. Kogalo iliwatandika vibaya wageni, hasa kwa kutilia maanani kuwa ilikuwa na makovu ya kupokezwa kichapo laini cha bao moja bila jibu ugenini jijini Juba wiki iliyopita. Sirkal iliizaba Al-Merreikh mabao 5-1 katika mechi ya marudiano na kujikatia tiketi ya kusogea mbele.
Gor Mahia sasa itachuana na miamba ya kandanda Misri, klabu ya Al-Ahly mnamo Septemba 13. Nayo klabu ya Polisi ya Kenya Jumapili iliwabandua wanakahawa wa Ethiopia nje ya mechi za Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuizaba bao moja kwa nunge katika Uwanja wa Abebe Bikila jijini Addis Ababa. Juma lililopita, timu hizo zilikabana koo na kutoa sare tasa. Maafande hao wa Kenya sasa wanatazamiwa kutoana udhia na Zamalek katika mchuano ujao wa hatua ya makundi.
Ligi ya EPL
Tunatamatisha kwa kuangazia matokeo ya baadhi ya mechi za karibuni kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza 'EPL'. Klabu ya Brighton iliendeleza ubabe wake dhidi ya Manchester United wikendi huku ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 nyumbani, huku nyota wake Danny Welbeck aking'ara zaidi. Ushindi huo ulikuwa ni wa nne kwa Brighton dhidi ya Man U katika mechi tano za mwisho walizokutana kwenye Ligi ya EPL, kwa hisani ya mabao ya Danny Welbeck na Joao Pedro huku lile la Manchester United likifungwa na Amad Diallo.
Kwengineko, nyota wa Chelsea Noni Madueke wikendi alifunga mabao 3 ya hat trick kwenye mchezo mwingine wa EPL ambao The Blues ilipata ushindi mnono dhidi ya Wolves kwenye Uwanja wa Molineux. Katika mchezo huo ambao Chelsea ilikuwa ugenini ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 6-2 ukiwa ni ushindi wao wa kwanza msimu huu baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Manchester City.
Katika matokeo mengine ya mechi za Ligi Kuu England, Bournemouth walitoka sare ya bao 1-1 na Newcastle, wakati ambapo Liverpool ilikuwa ikiisasambua Brentford mabao 2-0.
Mabao ya Leandro Trossard na Thomas Partey yalitosha kuipa Arsenal ushindi mwingine mnono, huku Wabeba Bunduki hao wakitulia katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 6, pointi sawa na Brighton na City waliomsimamia mabegani.
……………….TAMATI………….