Spoti, Sep 8
Hujambo mpenzi msikilizaji popote pale ulipo. Karibu tuangazie baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbali mbali za dunia. Nakusihi tuwe sote hadi tamati ya kipindi....
Karate Asia; Iran yaibuka ya 2
Iran imeibuka mshindi wa pili katika Mashindano ya Makadeti ya Shirikisho la Karate la Asia (AKF), kwa vijana wenye chini ya miaka 21. Timu hiyo ya Iran ilijinyakulia jumla ya medali 22, zikiwemo saba za dhahabu, tisa za fedha na sita za shaba kwenye mashindao hayo yaliyofanyika mjini Shaoguan, China kuanzia Septemba 5 hadi 7. Medali za dhahabu zilitwaliwa na Yalda Naghibeiranvand (kilo 50), Mehrnegar Ahmadi (chini ya kilo 61kg), Hananeh Salehi (+68kg), Ghazal Fathi (-48kg), Setayesh Ghaneifard (-54kg), Setayesh Afshar (+61kg), na Hossein kg Vafa (-67kg).

Medali za fedha ziliwaendea Mohammadjavad Safari (-75 kg), Abolfazl Hamdamjou (-60 kg), Fatemeh-Zahra Saeedabadi (-55 kg), Amir-Reza Mosalman (-61 kg), Mohammad Abdollahi (-61 kg), Aria Yousefi (-60 kg), Arshia Mihale (-68 kg), Aria Yousefi (-68 kg), Arshia Mihalei (-63 kg), na Faryar Bahadori (-70 kg). Zaidi ya hayo, Zahra Rezazadeh (kilo-53), Ava Farmani (kilo-47), Dina Karimi (kilo -61), na Mahan Mirzaei (+84kg) kila mmoja alipata medali ya shaba katika mashindano hayo. Zaidi ya makarateka mabarobaro 500 kutoka nchi 30 wameshiriki mashindano hayo ya siku tatu, wakilenga kutwaa mataji ya bara na kujidhihirisha kuwa nyota wa siku zijazo wa mchezo huo.
Soka Asia; Iran yaibinjua Guam
Timu ya soka ya vijana wa Iran iliinyoa kwa chupa, tena bila maji Guam kwa kuichabanga mabao 6-0 katika mechi za kuwania kufuzu kwa Kombe la Asia la AFC kwa vijana wenye chini ya miaka 23 la mwaka ujao 2026 Jumamosi. Alireza Safari aliwafungia vijana wa Uajemi bao la kwanza kunako dakika ya 43 na Kasra Taheri akamalizia hat trick kutoka dakika ya 47 hadi 78. Zikiwa zimesalia dakika sita, Saeid Saharkhizan alifunga bao la 5 kwenye mchezo huo wa Jumamosi uliopigwa katika Uwanja wa Al Nahyan mjini Abu Dhabi.

Mohammadjavad Hosseinnejad alipigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza Guam, kwa bao la sita katika dakika za lala salama. Iran, ambayo ilianza kampeni zake kwa ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Hong Kong, itakutana na Umoja wa Falme za Kiarabu Jumanne hii katika mchezo wao wa mwisho. Timu 44 ziligawanywa katika makundi 11 ya timu nne. Washindi wa kila kundi na washindi wa pili wa makundi hayo watafuzu kwa Kombe la Asia la AFC mwakani nchini Saudi Arabia.
Timu za Afrika zawania kutinga Kombe la Dunia 2026
Timu ya taifa ya soka ya Morocco imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika kutinga Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani FIFA la 2026 baada ya kuichakaza Niger mabao 5-0. Simba hao wa Atlas, ambao waliweka historia ya kutinga nusu fainali Kombe la Dunia la Qatar 2022, ilijua pointi tatu zingetosha kusonga mbele kwenye Kundi E ikiwa na michezo miwili tu, baada ya Tanzania kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Congo-Brazzaville mapema Ijumaa. Mchezaji wa Niger, Abdoul-Latif Goumey alitolewa nje kwa kosa la pili dakika ya 26 na Ismael Saibari alifunga krosi ya Youssef Belammari na kufunga bao dakika tatu baadaye. Saibari alifunga bao la pili kabla ya kipindi cha mapumziko alipoingiza mpira wa chini kutoka kwa Achraf Hakimi na Ayoub El Kaabi akafunga bao la tatu mapema kipindi cha pili kutoka kwa Belammari. Mshambulizi wa zamani wa Rangers, Hamza Igamane alitoka kwenye benchi na kufunga bao lake la kwanza la kimataifa kutokana na kona iliyopigwa vyema kabla ya Azzedine Ounahi kukamilisha kipigo hicho.

Ilikuwa jioni nzuri kwa Morocco walipocheza mechi ya kwanza katika Uwanja ulioboreshwa wa Prince Moulay Abdellah, ambao utaandaa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2025 Januari ijayo na kutumiwa wakati ufalme huo utakapoandaa pamoja Kombe la Dunia la 2030. Washindi wengine wanane wa makundi katika kufuzu kwa Afrika wamehakikishiwa kujiunga na Atlas Lions kwenye fainali za 2026, huku washindi wanne waliomaliza nafasi ya pili wakiingia katika mchujo wa kufuzu katika mashindano ya mabara. Taifa Stars ya Tanzania kama nilivyokudokeza ilitoa sare ya kufungana bao 1-1 na Congo Brazzaville katika mchezo mwingine wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026. Kwenye mchezo huo uliopigwa nchini Congo Brazzaville, wenyeji walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 68 mfungaji akiwa Dechan Moussavou, huku wenyeji wakiamini wangeibuka na ushindi, lakini Selemani Mwalimu aliisaiwazishia Staras dakika ya 84. Kutokana na matokeo hayo, Stars inaendelea kushika nafasi ya pili kwenye Kundi E ikiwa na pointi 10 kwa michezo sita, nyuma ya vinara Morocco wenye pointi 15 kwa michezo mitano. Congo Brazzaville inashika nafasi ya tano ikiwa na pointi moja kwa michezo sita, baada ya kupoteza michezo yote mitano ya mwanzo. Nayo Harambee Stars ya Kenya ilichabangwa mabao 3-1 na Gambia katika mechi yake ya kufuzu kwa Kombe la Dunia, matokeo ambayo yalififiliza matumaini yao ya kupata nafasi ya kufuzu kwa michuano hiyo ya dunia mwakani. The Scorpions waliduwaza kikosi cha Benni McCarthy, ambacho kilihitaji ushindi ili kuweka hai matumaini ya kutinga Kombe la Dunia.

Wachezaji wa Kenya wameapa kurekebisha mapungufu yao katika mechi zijazo. Huku hayo yakiarifiwa, mshambuliaji Allan Okello aliibuka nyota wa mechi wakati Uganda ilipoilaza Msumbiji mabao 4-0 uwanjani Namboole mnamo Ijumaa, huku Rogers Mato akifunga mara mbili. Mambo yaliwaendea segemnege zaidi Msumbiji baada ya kujifunga, na kuinyanyua Cranes hadi pointi 12 katika Kundi G la kufuzu kwa Kombe la Dunia la FIFA 2026. Katika mechi nyinginezo za karibuni za kuwania kufuzu Kombe la Dunia, Algeria siku ya Alkhamisi ya Septemba 4 iliichabanga Botswana mabao 3-1, huku Somalia ikinyolewa kwa chupa na Guinea katika mchezo wa Ijumaa uliopigwa Kampala, kwa kuchabangwa mabao 3-0.
Dondoo za Hapa na Pale
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania ameunga mkono wito wa kuondolewa timu ya waendesha baiskeli ya Israel kwenye mashindano ya mchezo huo yanayoendelea, kufuatia maandamano na malalamiko ya waungaji mkono wa Palestina nchini humo. Jose Manuel Albares ameeleza kutoridhishwa na ushiriki wa Israel kwenye mashindano hayo, akisisitiza kwamba ingawa anafadhilisha kutimuliwa kwa timu hiyo, lakini uamuzi wa mwisho ulikuwa wa Shirikisho la Kimataifa ya Uedeshaji Baiskeli (UCI), taasisi inayosimamia mchezo huo duniani. Albares alitoa ridhaa yake ya kufukuzwa timu ya Waisraeli ya Israel–Premier Tech kwenye mashindano hayo ya 'Vuelta a Espana' ya 2025 mnamo Jumatano. Matamshi yake yamekuja huku kukiwa na maandamano ya mara kwa mara ambayo yametatiza mashindano hayo, ikiwa ni pamoja na kufutwa kwa duru ya 5 na 11 ya mashindano hayo huko Bilbao na Figueres.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania amesisitiza kuwa, jamii ya kimataifa inapaswa kutuma ujumbe wa wazi kwa Israel katika kukabiliana na mauaji ya kimbari yanayoendelea huko Gaza. Wakati huo huo, bingwa wa Judo wa Ufaransa, Doria Boursas alikataa kupeana mkono na mwanariadha wa Israel Kerem Primo baada ya kumshinda katika robo fainali ya Mashindano ya Uropa ya Judo ya Vijana huko Bratislava. Boursas, ambaye hivi majuzi alitawazwa Bingwa wa Vijana wa Ufaransa katika kitengo cha chini ya kilo 63, alipata medali ya shaba baada ya maonyesho mengi ya nguvu. Aliona salamu ya kitamaduni ya kabla ya pambano lakini akakataa kupeana mkono mwishoni mwa pambano hilo - ishara ambayo, ikiwa ndani ya sheria, ilibeba mvuto mzito wa kisiasa.
Mbali na hayo, na kufuatia kukamatwa kwa Mahdieh Esfandiari, msichana wa Kiirani anayeishi Ufaransa na polisi ya nchi hiyo ya Ulaya kwa tuhuma za kuwaunga mkono watu wa Gaza, wanariadha 165 wa Kiirani wa kike na wa kiume wamemwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na kumtaka aingilie kati ya kuzuiliwa kinyume cha sheria na ubinadamu mwanamke huyo wa Iran.

Sehemu moja ya barua hiyo inasema, "Sisi, kikundi cha wanariadha wa Iran, tuna wasiwasi mkubwa kufuatia kukamatwa kinyume cha sheria kwa Bi. Mahdieh Esfandiari, raia wa Iran na mamlaka za Ufaransa tangu Februari 28, 2025, na kumweka katika kifungo cha upweke, kumweke vizuizi vikali vya kutangamana, na kunyimwa kupata huduma za matibabu."
Kwengineko, mwanamichezo wa Iran Zahra Kiani amejishindia medali ya kihistoria ya dhahabu katika Mashindano ya 17 ya Dunia ya Wushu mjini Brasilia nchini Brazil, ikiwa ni dhahabu ya kwanza kabisa kunyakuliwa na mwanawake wa Kiirani.

Kiani aliwachakaza washindani wake wote 27 na kuibuka kidedea kwenye kategoria ya Taolu ya mchezaji binafsi katika mashindano hayo ya dunia siku ya Jumamosi.
Na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limezindua rasmi Orodha ya Klabu Bora barani humo kwa mwaka 2025, ikiwa ni kigezo muhimu kabla ya Droo ya Awali ya Mashindano ya Kibara. Viwango hivyo vinaakisi utendaji wa klabu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho katika misimu mitano iliyopita, huku darubini ikielekezwa pia kwa mafanikio ya hivi majuzi. Klabu ya al-Ahly FC ya Misri inaendelea kuwa moto wa kuotea mbali barani humo, ikituama kileleni ikiwa na pointi 78, ikifuatiwa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini (pointi 62) na Espérance Sportive de Tunis ya Tunisia (pointi 57). RS Berkane ya Morocco (pointi 52) na Simba SC ya Tanzania (pointi 48) wakifunga orodha ya tano bora, kila klabu ikipiga hatua kubwa katika misimu ya hivi karibuni.
………………….TAMATI……….……..