Ulimwengu wa Spoti, Jan 27
(last modified Mon, 27 Jan 2025 08:37:14 GMT )
Jan 27, 2025 08:37 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Jan 27

Karibu tutupie jicho baadhi ya matukio makubwa ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa…..

Muiran bingwa kukwea barafu

Muirani Mohammadreza Safdarian aliibuka kidedea na kutwaa medali ya dhahabu katika fainali za Kombe la Dunia kwenye mchezo wa kukwea barafu. Raia wa Mongolia, Mandakhbayar Chuluunbaatar alishinda medali ya fedha baada ya kuibuka wa pili huku orodha ya tatu bora ikifungwa na Mkorea Kusini Joon Kyu Park aliyeshinda medali ya shaba.

Mohammadreza Safdarian aliyetwaa dhahabu

 

Duru ya pili ya mashindano hayo ya dunia yanayojulikana kwa Kimombo kama UIAA Ice Climbing World Cup, yalifanyika huko Saas-Fee, nchini Uswisi, kuanzia Januari 23 hadi 25.

Soka ya Ufukweni: Iran yainyuka Belarus

Timu ya soka ya ufukweni ya Iran ilivuna ushindi wa kishindo wa mabao 4-2 dhidi ya Belarus katika mechi ya kirafiki iliyosakatwa katika mji wa bandari wa Bushehr, katikati mwa nchi, Jumanne usiku. Saeid Piramoon, Ali Mirshekari, Abbas Rezaei, na Mehdi Shirmohammadi ndio walioifungia mabao Iran katika mechi hiyo ya kimataifa ya kirafiki.

 

Timu ya Iran iliishinda Belarus mabao 2-1 katika mechi yake ya kwanza na kupoteza kwa magoli 4-3 katika mechi ya pili. Timu ya soka ya pwani ya Iran inajiandaa kwa Kombe la Asia la Soka la Ufukweni la AFC 2025, linalotarajiwa kufanyika Machi 20 hadi 30 nchini Thailand. Iran imepangwa katika Kundi C pamoja na Imarati, Indonesia, na Afghanistan.

Katika hatua nyingine, Shirikisho la Soka la Ufukweni Duniani (BSWW) limewateua wachezaji 120 wa kiume, 50 wa kike na makocha 45 kwa ajili ya kupigiwa kura, ili kutafuta Nyota wa Mpira wa Ufukweni 2024. Wairani Ali Mirshekari, Amirhossein Akbari, Mehdi Shirmohammadi, Mohammadali Mokhtari na Mohammad Moradi ni miongoni mwa wanaowania Tuzo ya Mchezaji Bora kwa upande wa Wanaume. Hamid Behzadpour ameorodheshwa miongoni mwa Makipa Bora kwa Wanaume na Ali Naderi anachuania tuzo ya Kocha Bora. Washindi wa tuzo za mwaka huu wataamuliwa kwa kura kutoka kwa makocha na manahodha wa Vyama vyote vya Soka na Mashirikisho ya Soka la Ufukweni. Upigaji kura ulianza Alkhamisi, 23 Januari 2025 na manahodha na makocha watakuwa na hadi Februari 23 2025 kupiga kura zao. Washindi wa tuzo hizo tajwa watajulikana kwenye tamasha la Beach Soccer Stars gala 2024, huku tarehe na eneo vikitazamiwa kutangazwa hivi karibuni.

Karate: Binti wa Kiirani avuna dhahabu

Sara Bahmanyar wa Iran alishinda medali ya dhahabu katika Ligi Kuu ya Karate 1 ya 2025 iliyofanyika Paris, Ufaransa. Alimshinda mtani wake Masoumeh Mohsenian kwa alama 6-3 katika mpambano wa fainali ya Kumite kwa wenye uzani wa kilo 50. Aidha Ali Meskini wa Iran alimshinda raia wa Albania Orges Arifi kwa pointi 9-6 katika mechi ya kuwania medali ya shaba kwa upande wa wanaume wenye kilo 60. Makarateka zaidi ya400 kutoka nchi 70 walishiriki katika mashindano hayo ya kifahari kuanzia Januari 24 hadi 26. Mji wa Hangzhou, China, unatazamiwa kuandaa mashindano ya pili ya msimu wa 2025 wa Ligi Kuu ya Karate 1 kuanzia Machi 14 hadi 16.

Soka Afrika

Klabu ya Yanga ya Tazania imefuzu kibabe katika mduara wa 32 bora kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho. Wananchi waliigaraza Copco ya Mwanza mabao 5-0 kwenye mchuano wa wikendi uliopigwa katika Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam, na kuvuna ushindi mnono ambao umewatuliza mashabiki wake, waliolilia chooni baada ya timu hiyo kubanduliwa kkwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Mambo yalikuwa hivi katika Uwanja wa KMC jijini Dar. Kwa ushindi huo, Yanga inakuwa timu ya 31 kutinga hatua ya 32 bora.

 

Wakati huo huo, watani wao, klabu ya Simba siku ya Jumapili walishuka dimbani kuvaana na Kilimanjaro, na kama ilivyotarajiwa, Wekundu wa Msimbazi wangurumapo, nani na ubavu wa kuwakaribia? Simba imeshinda mchuano huo wa Federation Cup kwa jumla ya magoli 6-0, wafungaji wakiwa ni Valentino Mashaka, Ladack Chasambi, Joshua Mutale, Stephen Mukwala, Edwin Balua na goli la kujifunga la Patrick Sebastian.

Mashabiki wa Simba wakifurahia ushindi

 

Simba ipo katika msururu wa kuvuna ushindi, kwani iliingia kwenye mechi hiyo ya Jumapili, ikiwa tayari imefuzu kibabe hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kuifunga CS Constantine ya Algeria mabao 2-0, na kuongoza kundi A kwa kufikisha pointi 13 ikiwaacha Waarabu hao nafasi ya pili na alama 12.

Katika hatua nyingine, Congo Brazzaville imeondolewa kushiriki michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) inayotarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu. Michuano hiyo itafanyikia nchini Kenya, Uganda na Tanzania katika tarehe ambazo bado hazijaanishwa. Nafasi ya Congo Brazaville waliokuwa Kundi D pamoja na Nigeria, Sudan na Senegal imechukuliwa na Equatorial Guinea. Kutolewa kwao kunafuatia madai kwamba walimchezesha mchezaji asiyestahili, mshambuliaji Japhet Eloi Mankou Nguembete. Kadhalika Shirikisho la Soka la Congo Brazaville limepigwa faini ya Dola za 10,000 za US ambayo inatakiwa kulipwa ndani ya siku 60.

Dondoo za Hapa na Pale

Kocha mkuu mpya aliyeteuliwa hivi karibuni wa Persepolis ameelezea matumaini yake ya kushinda ligi. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 63 aliitwa Persepolis siku ya Ijumaa na alisafiri hadi Tehran Jumamosi asubuhi. Ismail Kartal amesaini mkataba wa miezi 18 na Wekundu wa Tehran. Anachukua nafasi ya kocha wa Uhispania Juan Carlos Garrido kwa muda uliosalia hadi kumalizika msimu. Anasema, "Menejimenti ya Persepolis imekuwa ikiwasiliana nami kwa muda. Nilifanya uchunguzi wa kina na kugundua kuwa Persepolis ni moja ya klabu maarufu nchini Iran. Timu hiyo ina idadi kubwa ya mashabiki, na watazamaji 40,000 hadi 50,000 wanahudhuria kila mechi.

Klabu ya soka ya Persepolis

Kwa sasa wako katika nafasi ya nne kwenye ligi ya Irani na pia wanashindana katika Ligi ya Mabingwa ya AFC Elite.”

Kwengineko, Barcelona iliishukia vibaya Valencia na kuigaragaza mabao 7-1 kakika mchuano wa wikendi wa Ligi Kuu ya Soka ya Uhispania (La Liga). Magoli ya Barca kwenye ngoma hiyo ya kiutu uzima yalifungwa na Fermin Lopez aliyecheka na nyavu mara mbili, Lewandowski, Raphinha, Frenkie de Jong, Ferran Torres, huku Cesar Tarrega akijifunga la kisigino.

Wakati huo huo, Kylian Mbappe alifunga hat-trick yake ya kwanza kwa Real Madrid Jumamosi huku mabingwa hao wa La Liga wakiichapa kwa urahisi klabu ya Real Valladolid mabao 3-0, na kuendeleza uongozi wao kileleni mwa msimamo.

Na nikudokeze tu kwamba, Madrid imekuwa klabu ya kwanza kabisa ya soka kuwa na mapato ya zaidi ya Yuro bilioni moja kwa mwaka, hayo ni kwa mujibu wa tathmini ya kampuni ya Deloitte. Real wamesalia kileleni mwa ligi hiyo kifedha wakiwa na mapato ya Yuro bilioni 1.05 kwenye msimu wa 2023-2024 ambapo walitawala La Liga na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Manchester City wameshupalia nafasi ya pili wakiwa na mapato ya Yuro milioni 838 huku Paris Saint-Germain PSG, Manchester United, na Bayern Munich, wakifunga nafasi tano za kwanza kwenye ligi hiyo.

……………..TAMATI………..