Jul 20, 2023 11:40 UTC
  • Amir Abdollahian: Tumepokea mapendekezo ya Oman ili kurejesha pande zote katika JCPOA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuhusu mazungumzo yake na mwenzake wa Oman kwamba: Muscat inafanya juhudi za kukurubisha mitazamo ili pande zote husika zirejee katika utekelezaji wa majukumu yake katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Sayyid Badr Albusaidi Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman aliyeko ziyarani mjini Tehran amekutana na kufanya mazungumzo na Hossein  Amir- Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.  

Hossein Amir-Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezungumzia ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman hapa Tehran na masuala mbalimbali yaliyojadiliwa katika mazungumzo ya pande mbili na kusema: Ajenda kuu ya mazungumzo ya pande mbili za Iran na Oman ilihusu ufuatiliaji wa mapatano na hati zilizosainiwa katika mazungumzo ya viongozi wa nchi mbili mwaka mmoja uliopita. 

Amir Abdollahian pia amesema: Katika mazungumzo ya pande mbili Tumependekeza kuuanzishwa kongamano la mazungumzo na ushirikiano wa kikanda wa nchi za Ghuba ya Uajemi (majirani 6 wa kusini na majirani 2 wa kaskazini yaani Iraq na Iran) na pengine nchi ya Yemen inaweza kuongezwa katika mchakato huu.

Mazungumzo ya ujumbe wa Iran na Oman mjini Tehran 

Katika miongo kadhaa ya karibuni Iran na Oman daima zimekuwa na uhusiano nzuri unaotilia mkazo suala la kuheshimiana na kujali maslahi ya pande mbili, licha ya mivutano iliyojitokeza katika Ghuba ya Uajemi na njama za Marekani za kuzidisha chuki na propaganda chafu dhidi ya Iran. 

Viongozi wa Oman wanaamini kuwa uhusiano wa karibu wa nchi hiyo na Iran umejengeka kwa msingi wa ukweli na  uhalisia wa mambo na wanaitambua Iran  kuwa ni nchi kubwa jirani. Aidha nchi zote mbili hazina hitilafu yoyote katika suala la ardhi au mipaka.

Tags