Afisa mwandamizi wa usalama wa Iran ahudhuria mkutano wa BRICS Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i100270-afisa_mwandamizi_wa_usalama_wa_iran_ahudhuria_mkutano_wa_brics_afrika_kusini
Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Iran yuko nchini Afrika Kusini kushiriki mkutano wa ngazi ya juu wa usalama wa nchi kundi la BRICS.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 24, 2023 08:02 UTC
  • Afisa mwandamizi wa usalama wa Iran ahudhuria mkutano wa BRICS Afrika Kusini

Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Iran yuko nchini Afrika Kusini kushiriki mkutano wa ngazi ya juu wa usalama wa nchi kundi la BRICS.

Ali-Akbar Ahmadian amewasili Pretoria, Afrika Kusini leo Jumatatu kushiriki mkutano huo wa siku tatu wa Washauri wa Usalama wa Taifa (NSA) wa nchi wanachama wa kundi la BRICS.

Ahmadian anatazamiwa kufanya vikao na maafisa wenzake wa usalama wa kundi la BRICS, pambizoni mwa duru ya 13 ya mkutano huo wa Washauri wa Usalama wa Taifa (NSA) wa jumuiya hiyo ya nchi zinazoibukia kiuchumi.

Mkutano huo wa usalama unajiri mwezi mmoja kabla ya kufanyika mkutano ujao wa kilele wa viongozi wa nchi wanachama wa kundi la BRICS utakaofanyika mjini Johannesburg, kuanzia Agosti 22 hadi 24 mwaka huu 2023.

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amealikwa rasmi kuhudhuria mkutano huo wa kundi la BRICS mwezi ujao. Hivi karibuni, Rais wa Iran alisema Jamhuri ya Kiislamu inaweza kuwa mshirika endelevu wa kuunganisha nchi wanachama wa BRICS katika maeneo muhimu ya kupitisha nishati na masoko makubwa duniani, kwa kuzingatia nafasi yake ya kipekee ya jiografia ya kisiasa na jiografia ya kiuchumi.

Mkutano wa BRICS uliofanyika mwezi uliopita Afrika Kusini

Kwa mujibu wa Sayyid Raisi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetimiza vigezo vyote vya kukubaliwa kuwa mwanachama wa kundi hilo la BRICS.

Aidha Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran karibuni alienda Cape Town nchini Afrika Kusini, kwa ajili ya kushiriki mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa kundi la BRICS.