Iran na Afrika Kusini katika mkondo wa kuhuisha kikamilifu mahusiano
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wiki hii aliekea Pretoria Afrika Kusini kwa ajili ya kushiriki katika mkutano wa 15 wa Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Iran na Afrika Kusini na kukutana na viongozi mbalimbali wa taifa hilo.
Alkhamisi ya jana 10 Agosti, Hussein Amir Abdollahian alikutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Naledi Pando, Waziri wa Mashauri ya Kigeni na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini ambapo wawili hao walijadiliana na kubadilishana mawazo kuhusiana na uhusiano wa pande mbili.
Kikao cha Kamisheni ya Panoja ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Afrika Kusini kinafanyika baada ya kusimama kwa miaka mitatu kutokana na janga la corona. Kufuatilia masuala ya pande mbili na baadhi ya masuala ya kimataifa, pamoja na kukutana na Rais wa Afrika Kusini, ni miongoni mwa malengo makuu ya safari ya Amir Abdollahian katika nchi hiyo muhimu ya Kiafrika.

Mkutano wa 15 wa Kamisheni ya Pamoja ya Iran na Afrika Kusini ulianza Jumanne ya tarehe 8 Agosti ambapo moja ya mipango ya kamisheni hii ni kukamilisha mikataba na hati za ushirikiano baina ya pande mbili kwa ajili ya kutiwa saini katika safari ijayo Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Afrika Kusini, itakayofanyika baadaye muda si mrefu.
Uhusiano kati ya Iran na Afrika Kusini uko katika kiwango cha juu na chenye uratibu. Mataifa haya mawili yamekuwa amilifu katika asasi muhimu za kimataifa kama Umoja wa Mataifa au Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA). Iran na Afrika Kusini sanjari na kupinga vikwazo vya upande mmoja, zimekuwa NA misimamo takribani inayofanana kuhusiana na masuala mengi ya eneo la Asia Magharibi.
Wakati huo huo, serikali ya awamu ya 3 ya Iran baada ya majirani na mataifa ya eneo imekuwa ikiipa kipaumbele Afrika katika sera zake za kigeni. Safari ya hivi karibuni ya Seyyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nchi tatu za Kenya, Uganda na Zimbabwe na kutiliana saini mikataba kadhaa ya kiuchumi na kibiashara na nchi hizo ni ithbati ya utendaji huu wa serikali ya awamu ya 13 wa kulipa umuhimu bara la Afrika.
Afrika Kusini ni mojawapo ya nchi zinazoongoza kimaendeleo kati ya nchi 55 za Afrika, na zaidi ya asilimia 20 ya kiwango cha biashara ya nje ya bara la Afrika inashikiliwa na taifa hili.

Kutokana na nia na azma thabiti ya viongozi wa Iran na Afrika Kusini ya kupanua ushirikiano, mahusiano ya kibiashara kati ya nchi hizi mbili yamechukua wigo mpana zaidi katika miaka ya hivi karibuni. Takwimu zinaonyesha kuwa, katika miaka miwili ya hivi karibuni, Afrika Kusini imekuwa soko la kwanza kwa mauzo ya bidhaa za Iran barani Afrika.
Uwezo wa kiuchumi hususan katika nyanja za mafuta na madini na uhusiano mzuri wa kisiasa na mitazamo ya pamoja ya nchi hizo mbili kuhusu masuala mengi ya kimataifa likiwemo suala la Palestina, haja ya kuangaliwa upya muundo wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la umoja huo, vita dhidi ya ugaidi, matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia na ushirikiano katika asasi na jumuiya za kikanda na kimataifa kama vile BRICS, ni mambo ambayo yanaandaa mazingiwa mwafaka ya kustawishwa zaidi uhusiano wa Tehran na Pretoria hususan katika nyuga za kibiashara na kiuchumi.

Tangu mwaka 1995, hadi sasa kumetiwa saini mikataba 25 kati ya Iran na Afrika Kusini, na hivi sasa baadhi ya mikataba hiyo iko kwenye ajenda ya wataalamu wa nchi mbili ili kukamilishwa.
Ni kwa muktadha huo, ndio maana iinatarajiwa kuwa, kufanyika mkutano wa 15 wa Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya nchi hizo mbili kutaharakisha utekelezaji wa mikataba hiyo pamoja na kutiwa saini mikataba mipya kwa minajili ya kuongeza ushirikiano kati ya nchi hizi mbili. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kuhusiana na suala hilo kwamba: Kuhuishwa kikamilifu uhusiano na Afrika Kusini ni jambo ambalo lipo katika ajenda za kufanyiwa kazi.