Salami: Vitisho dhidi ya Iran vinazidi kufupisha uhai wa Israel
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ameionya Israel na kusema kuwa, vitisho vya Tel Aviv dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran havitakuwa na matokeo mengine isipokuwa kuendelea kufupisha uhai wa utawala wa Kizayuni.
Meja Jenerali Hossein Salami amesema hayo katika mkutano wake na wadau katika sekta ya mitandao na teknolojia ya dijitali, siku tatu baada ya David Barnea, Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Israel (Mossad) kutoa vitisho kuwa Israel itawaua maafisa wa ngazi za juu wa Iran katikati ya Tehran.
Salami amesema, "Wazayuni wanaandamwa na matatizo mengi, na alama za kuporomoka kwao zipo wazi kabisa. Kwa msingi huo, hivi sasa wamegeukia bwabwaja na vitisho hewa vya kuwaua kigaidi makamanda wetu."
Kamanda Salami ameuhutubu utawala wa Kizayuni kwa kusema: Mnapaswa kufahamu kuwa, mkitoa vitisho dhidi ya usalama wa Iran, tutakuwa na machaguo mengi, na maisha yenu yatakatizwa.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, nguvu na uwezo mkubwa wa Iran umeifanya Jamhuri ya Kiislamu isiburuzwe au kusalimu amri mbele ya madola makubwa na kuongeza kuwa, stratejia za maadui za kulitenga taifa hili zimefeli na kugonga mwamba.
Hivi karibuni pia, Brigedia Jenerali Abbas Nilforoushan, Naibu Kamanda wa Operesheni za SEPAH alifichua mpango wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuunda makombora mapya ya hypersonic ambayo alisisitiza kuwa yataufanya utawala wa Kizayuni ulipe gharama kubwa.
Alisema teknolojia ya Iran ina uwezo wa kuboresha na kuyaongeza nguvu makombora yake ya balestiki yaweze kupiga hadi umbali wa kilomita 2,000.