"Muungano madhubuti umeundwa dhidi ya Wazayuni duniani"
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i102436-muungano_madhubuti_umeundwa_dhidi_ya_wazayuni_duniani
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema muungano thabiti na wenye nguvu umeundwa duniani dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 19, 2023 22:53 UTC

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema muungano thabiti na wenye nguvu umeundwa duniani dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Meja Jenerali Hossein Salami alisema hayo jana Jumanne katika mkutano wa 'Dunia Mpya' uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kaskazini mwa Tehran na kuongeza kuwa, kambi ya muqawama hivi sasa ipo katika hali tofauti kinyume na huko nyuma.

Meja Jenerali Salami ameeleza bayana kuwa, eneo la Asia Magharibi umekuwa uwanja wa uhasama na makabiliano baina ya madola makubwa na kusisitiza kuwa, kutokana na nafasi yake ya kijiografia na kuwa na rasilimali nyingi, madola la kikoloni yamekuwa likilitazama eneo hili kwa jicho la tamaa.

Amesema, "Hii leo, Mapinduzi ya Kiislamu yanakabiliana na adui mashariki mwa Bahari ya Mediterrania, na kaskazini mwa Bahari Nyekundu."

"Jiografia ya Mapinduzi ya Kiislamu imetanuka zaidi, na tuna kambi nyingi waitifaki, kama Hizbullah ya Lebanon, ambayo ina uwezo wa kuamua mlingano wa nguvu katika nyuga za siasa na usalama katika eneo," ameongeza Salami.

Nembo za harakati za muqawama katika eneo

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, nguvu na uwezo mkubwa wa Iran umeifanya Jamhuri ya Kiislamu isiburuzwe au kusalimu amri mbele ya madola makubwa na kuongeza kuwa, stratejia za maadui za kulitenga taifa hili zimefeli na kugonga mwamba. 

Meja Jenerali Hossein Salami ameongeza kuwa, "Kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu, hakukuwa na alama zozote za mapambano huko Palestina, lakini hii leo, makundi ya Palestina yamewasha moto katika maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu, na kuwakosesha usingizi Wazayuni."