Sep 25, 2023 09:16 UTC
  • Mikutano ya kidiplomasia New York; fursa ya kubainishwa diplomasia ya Iran

Hossein Amir Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kufanyika vikao na mazungumzo na viongozi wa nchi mbalimbali pambizoni mwa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kumeandaa uwanja wa kuimarishwa diplomasia ya Iran ulimwenguni.

Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa bado unaendelea huko New York, Marekani. Hossein Amir Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye bado yuko mjini New York anaendelea kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi na taasisi mbalimbali duniani. Kufanyika vikao vya Baraza Kuu, huandaa fursa kwa ajili ya kufanyika mikutano na mazungumzo ya viongozi mbalimbali duniani. Kwa hakika, pamoja na kuwepo mapungufu ya kimuundo ya Umoja wa Mataifa, mkutano wa Baraza Kuu huandaa uwanja  kwa marais, mawaziri wa mambo ya nje na viongozi wa nchi mbalimbali kuweza kubainisha kwa uwazi zaidi mitazamo ya nchi zao kuhusiana na masuala mbalimbali ya kimataifa.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa nchi ambazo hasa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya zinaeneza siasa chafu na za kiuadui dhidi yake duniani na Rais Ebrahim Raisi wa Iran, pia aliashiria wazi suala hilo kwenye hatuba yake katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Katika mikutano na vikao vyao vya kidiplomasia huko New York, Raisi na Amir Abdollahian walijaribu kupunguza makali ya siasa hizo za chuki dhidi ya mfumo wa Kiislamu kwa kubaini siasa na sera za  Iran na hivyo kupelekea kushindwa siasa za maadui za kutaka kuitenga Iran.

Aidha rais na waziri wa mambo ya nje wa Iran wametumia mikutano ya kidiplomasia mjini New York kama fursa na jukwaa la kuunga mkono amani na kuboresha suala la kufanyika mazungumzo duniani. Mazungumzo ya Amir Abdollahian na Sameh Shoukry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, ambayo yalifanyika katika mazingira ya kirafiki, yanaweza kutathminiwa katika mtazamo huo.

Vilevile, mikutano na vikao vinavyoendelea kufanyika huko New York na vyombo vya habari pamoja na jumuiya za kielimu vinatoa fursa ya kuimarishwa, kutazamwa upya au kubainishwa kimataifa siasa halisi za nchi. Jukwa hilo huandaa uwanja mzuri kwa wachambuzi, wahadhiri na wasomi kwa ajili ya kukutana moja kwa moja na viongozi wa nchi mbalimbali na hivyo kuweza kufahamu sera na mitazamo ya nchi hizo. Katika safari yake huko New York Rais Ebrahim Raisi alifanya vikao kadhaa na vyombo vya habari na kielimu  na kuelezea sera za kigeni za serikali yake ya 13.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na waandishi wa habari

Masuala yaliyopewa kipaumbele muhimu katika mazungumzo ya Rais na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ni kuwa Tehran inakaribisha mazungumzo ya pande zote, kuwepo amani  duniani, kutetea haki za wanawake, inataka kulindwa na kuheshimiwa haki na maslahi ya nchi dhaifu pamoja na kutekelezwa siasa na hatua za kukabiliana na ugaidi na migogoro mbalimbali duniani. Wakati huohuo inakaribisha na kuzingatia suala la kuwepo uhusiano mzuri na nchi njirani.

Kwa hivyo, tunaweza kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kinyume na baadhi ya nchi zinazotumia jukwa la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kueneza chuki na vitisho dhidi ya mataifa mengine, daima imekuwa ikitilia mkazo suala la amani na kuungwa mkono wanyonge na wanaodhulumiwa duniani.

Ijapokuwa Umoja wa Mataifa uko chini ya ushawishi wa nchi za Magharibi na unaegemea kwenye sera za Marekani, mkutano wa Baraza Kuu na vikao vya pembeni vinaweza kutumika katika kubainisha wa kukuza siasa  na sera za nchi, suala ambalo rais wa Iran alilisisitiza na kuliweka wazi katika mikutano na vikao vyake na vyombo vya habari vya Marekani.