Rais wa Iran: Ikiwa mauaji ya watu wa Gaza hayatasitishwa, vita vitaenea
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i103514-rais_wa_iran_ikiwa_mauaji_ya_watu_wa_gaza_hayatasitishwa_vita_vitaenea
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mazungumzo na Rais wa Ufaransa kuwa, ikiwa jinai za utawala wa Kizayuni ikiwemo mauaji ya raia na kuuzingira Ukanda wa Ghaza hayatasitishwa, hali ya mambo itakuwa tete zaidi na vita vitaenea.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 15, 2023 11:48 UTC
  • Rais wa Iran: Ikiwa mauaji ya watu wa Gaza hayatasitishwa, vita vitaenea

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mazungumzo na Rais wa Ufaransa kuwa, ikiwa jinai za utawala wa Kizayuni ikiwemo mauaji ya raia na kuuzingira Ukanda wa Ghaza hayatasitishwa, hali ya mambo itakuwa tete zaidi na vita vitaenea.

Muhammad Jamshidi Naibu Afisa wa Masuala ya Kisiasa katika Ofisi ya Rais wa Iran amedokeza kuhusu mazungumzo ya simu kati ya Rais Ebrahim Raisi wa Iran na Emmanuel Macron Rais wa Ufaransa kuwa: Rais Raisi amejibu simu ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kwa kusema, iwapo jinai za utawala wa Kizayuni yakiwemo mauaji ya raia na kuzingirwa Ghaza hazitasitishwa basi hali ya mambo itakuwa tete zaidi na vita vitapanuka.   

Jinai za Israel katika Ukanda wa Ghaza 

Utawala haramu uwa Kizayuni umeanzisha mashambulizi dhidi ya Ukanda wa Ghaza baada ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) tarehe 7 mwezi huu wa Oktoba kutekeleza oparesheni kwa jina la "Kimbunga cha Al Aqsa" dhidi ya utawala ghasibu wa Israel; ambapo hadi sasa mashambulizi hayo bado yanaendelea. 

Utawala wa Kizayuni ambao siku kadhaa zilizopita ulishindwa kwa fedheha katika medani ya vita kati yake na muqawama wa Palestina umetekeleza hatua isiyo ya kibinadamu kwa kufunga vivuko vyote vya Ukanda wa Ghaza ili kuwalazimisha wanamapambano wa Palestina kusimamisha oparesheni ya kijasiri ya Kimbunga cha Al Aqsa. 

Umoja wa Mataifa Alhamisi iliyopita ulitangaza kuwa jeshi la Israel limeutaarifu kwamba jamii nzima ya wakazi wa kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza inapasa kuondoka katika eneo hilo na kuelekea kusini kwa Ghaza katika muda wa masaa 24, hata hivyo msemaji wa wanajeshi wa utawala huo ghasibu ametangaza kuwa muhula uliotolewa huenda usifuatwe.