BRICS, kwa ombi la Iran, kufanya mkutano wa dharura kujadili Gaza
(last modified Tue, 21 Nov 2023 03:16:18 GMT )
Nov 21, 2023 03:16 UTC
  • BRICS, kwa ombi la Iran, kufanya mkutano wa dharura kujadili Gaza

Kufuatia pendekezo la Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kundi la BRICS linatazamiwa kufanya mkutano wa dharura kujadili vita vya uvamizi vya Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini imesema katika taarifa kuwa: Viongozi wa nchi za BRICS-Brazil, Russia, India na China - watakutana kwa mkutano wa dharura utakaofanyika kwa njia ya intaneti, kwa ajili ya kujadili kadhia ya Gaza.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, Rais  Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, anatazamiwa leo Jumanne kutoa hotuba ya ufunguzi wa kikao hicho cha dharura cha nchi za BRICS kujadili mashambulizi ya kikatili ya Israel dhidi ya Gaza.

Afrika Kusini inakuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kujadili njia za kukomesha jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Gaza, kwa kuwa ndiye mwenyekiti wa kiduru wa kundi la madola yanayoinukia kiuchumu la BRICS.

Taarifa ya Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini imebainisha kuwa, viongozi wa wanachama wapya wa BRICS wamealikwa pia kushiriki mkutano huo. Wanachama wapya wa BRICS ni pamoja na Saudi Arabia, Argentina, Misri, Ethiopia, Iran na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Jinai za Israel zisivyosaza hata watoto wadogo huko Gaza

Kadhalika Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres anatazamiwa kushiriki mkutano huo utakaofanyika kwa njia ya mtandao, ambapo mwishowe washiriki watatoa taarifa ya pamoja.

Hii ni katika hali ambayo, Idara ya Habari ya Serikali ya Gaza imesema kuwa, Wapalestina 13,300, wakiwemo watoto wasiopungua 5,600 na wanawake 3,550 wameuawa shahidi tokea utawala haramu wa Israel uanzishe vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 7.