Iran na Cuba mbioni kuimarisha uhusiano wa kimkakati
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i105632-iran_na_cuba_mbioni_kuimarisha_uhusiano_wa_kimkakati
Marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Cuba wametiliana saini hati 7 za ushirikiano zinazolenga kuimarisha uhusiano wa kimkakati baina ya pande mbili.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Dec 05, 2023 05:54 UTC
  • Iran na Cuba mbioni kuimarisha uhusiano wa kimkakati

Marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Cuba wametiliana saini hati 7 za ushirikiano zinazolenga kuimarisha uhusiano wa kimkakati baina ya pande mbili.

Rais wa Jamhuri ya Cuba ambaye anaongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa kisiasa na kiuchumi wa nchi yake Jumapili ya juzi aliwasili hapa mjini Tehran kwa mwaliko rasmi wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Jumatatu ya jana kiongozi huyo wa Cuba alikutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Ebrahim Raisi na baadaye alasiri akakutana na kufanya mazungumzo na Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Rais Miguel Díaz-Canel wa Cuba, amefanya safari nchini Iran ikiwa imepita miaka 22 baada ya ziara ya mwisho ya hayati Rais Fidel Castro mjini Tehran.

Hati za ushirikiano zilizotiwa Saini hapo jana baina ya Cuba na Iran zinajumuisha nyuga mbalimbali za kielimu, kiteknolojia, sekta ya afya, kilimo, nishati, madini, mawasiliano na tiba.

Sayyid Ebrahim Raisi amesema katika hafla ya utiaji Saini hati hizo za makubaliano ya ushirikiano kwamba:  Leo kumefunguliwa ukurasa mpya katika mahusiano ya Iran na Cuba suala ambalo litapelekea kupanuliwa na kustawishwa zaidi ushirikiano wa pande mbili.

Mwaka huu (2023) Rais Ebrahim Raisi katika fremu ya safari ya kieneo ya eneo la Amerika ya Latin alifanya safari Havana mji mkuu wa Cuba akiitikia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo Miguel Díaz-Canel. Safari hiyo ya Ebrahim Rais nchini Cuba ilifanyika ikiwa imepita pia miaka 12 tangu kufanyika kwa safari ya mwisho ya Rais wa Iran katika nchi hiyo. Katika safari hiyo kulitiwa Saini hati 6 za ushirikiano katika sekta mbalimbali kama za kimahakama, ushirikiano jumuishi wa kisiasa, ushuru na forodha na katika uga wa teknolojia ya taarifa.

Marais wa Iran na Cuba

 

Serikali ya awamu ya 13 inayoongozwa na Sayyid Ebrahim Raisi mbali na kutoa kipauumbele kwa mataifa ya Kiislamu na majirani imekuwa ikitilia mkazo pia katika sera zake za kigeni juu ya kupanua ushirikiano na mataifa ambayo yanaendana nayo kimsimamo kama Cuba. Iran na Cuba yakiwa mataifa mawili licha ya kuwa mbali kijiografiaa lakini yana malengo ya pamoja yana mambo yanayoshirikiana kama vile kupigania mamlaka ya kujitawala, kutokubali kusalimu amri mbele ya ubeberu na kuunga mkono harakati za kupigania uhuru. Hapana shaka kuwa, haya ni baadhi ya mambo ambayo yameyafanya mataifa haya mawili kuwa na ukuruba wa kisiasa na kiuchumi baina yao.

Uhusiano wa Iran na Cuba uliimarika zaidi baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979 na Iran kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM)  ambapo wanachama wake walikuwa na misimamo inayoshabihiana ya kupinga ubeberu. Hivi sasa uhusiano huo unaendelea katika nyuga mbalimbali.

Kupambana na sera za Marekani za kuingiliana masuala ya ndani ya mataifa mengine ni moja ya maudhui ambazo zinahesabiwa kuwa Tehran na Havana zinashirikaiana katika hilo. Kuanzia mwanzoni mwa muongo wa 60, Marekani iliiwekea vikwazo nchi hiyo kutokana na hatua yake ya kufuata siasa za kimapinduzi na za kujitegemaa na kutokubali kuburuzwa na Washington. Vikwazo hivyo baadaye vilichukua wigo mpana zaidi. Kuanzia mwaka 1980 na baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu sera hizo za Marekani za uraibu wa vikwazo zilianza kutekelezwa dhidi ya Iran.

Licha ya Iran na Cuba kuandamwa na vikwazo na mibinyo ya kila namna lakini mataifa haya yameweza kuwa kiigizo kilichofanikiwa katika uga wa kutegemea nguvu ya ndani na kusambaratisha siasa za vikwazo za Marekani.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari akiwa na mgeni wake, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisisitiza kuwa: Muqawama dhidi ya satwa na mfumo wa kibeberu ni jambo la pamoja la Iran na Cuba ambalo limeziweka nchi hizo mbili kuandamwa na vikwazo vya Marekani.

Marais wa Iran na Cuba walipokutana Havana huko Cuba miezi kadhaa iliyopita

 

Akiashiria kwamba Iran na Cuba zimewekewa vikwazo na Marekani kutokana na kusimama kwao kidete dhidi ya upendaji makuu wa Marekani ameongeza kuwa, Marekani na mfumo wa kibeberu wanadhani kwamba kwa kuweka vikwazo, wanaweza kuyalazimisha mataifa yaliyoamua kusimama kidete dhidi ya ubeberu yasalimu amri au kulegeza kamba, huu ni mghafala wa mfumo kibeberu na ni kwenda kombo katika mahesabu yao. Kuimarisha uhusiano wa nchi ambazo ziko katika hali ya vikwazo kunaweza kusambaratisha vikwazo hivyo.

Hata hivyo tunapaswa kuashiria nukta hii kwamba, licha ya uhusiano mkongwe baina ya Iran na Cuba lakini ushirikiano wa kibiashara baina ya mataifa haya mawili ni mdogo kiasi kwamba, Cuba inahesabiwa kuwa, mshirika waa 157 wa Iran katika uga wa kibiashara. Filihali hati kadhaa za ushirikiano baina ya Tehran na Havana katika uga wa kidiplomasia na kihuduma zimo katika hali ya kutekelezwa. Licha ya kuweko kiwango kidogo cha mabadilishano ya kibiashhara, lakini ushirikiano wa Iran na Cuba katika uga wa ulinzi, taarifa na tiba umo katika hali ya kupanuka na kuchukua wigo mpana zaidi.

Ni jambo lisilo na shaka kuwa, hati zilizotiwa Saini jana (Jumatatu) baina ya pande mbili zitapiga jeki juhudi za kupanua ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na kusahilisha mahusiano ya mashirika ya pande mbili.

Ni wazi kuwa, katika uhusiano wa kiuchumi kati ya Iran na Cuba kuna fursa za uwekezaji wa pamoja katika sekta za chakula, dawa, madini, nishati na utalii, na matakwa ya mamlaka za nchi hizo mbili pia ni kuendeleza ushirikiano. Rais wa Cuba pia ametathmini ziara yake rasmi nchini Iran kama "fursa ya kuendelea kuimarisha uhusiano katika nyanja mbalimbali kwa manufaa ya mataifa yote mawili".